NA KAIS MUSSA KAIS.
MWENYEKITI Mwenza wa Ukawa na Mwenyekiti wa chama cha NLD, Emmanuel
Makaidi amefariki dunia leo mchana kwa shinikizo la damu akiwa Hospitali
ya Nyangao mkoani Lindi.
Wasifu wake
Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Alianza
elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka
1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle
school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph
na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha tano na sita) katika
Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka 1957 – 1958. Baada ya
hapo alielekea Afrika Kusini na kujiunga na Chuo Kikuu cha Witwatersrand
na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya mwaka 1958 –
1960.
Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea kupata ufadhili wa
masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea Marekani na kusoma
masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya uzamili kati ya mwaka
1960 – 1962.
Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha Howard kilichoko jijini Washington,
Marekani. Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza
kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu,
katika kitengo cha Utumishi. Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili).
Alirudi tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika
Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard. Aliporejea nchini kwa
mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka
1985 alipopewa kazi nyingine kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na
Mishahara kwenye kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma
nchini.
Baada ya hapo aliendelea na kazi serikalini ila kuanzia mwaka 1992
hadi mauti yanamfika, Dk Makaidi hajajishughulisha tena na kazi za
serikalini wala mashirika binafsi.
Alikuwa amejiajiri akiwa na kampuni kadhaa zilizoajiri Watanzania wa
vipato vya kawaida, lakini pia alikuwa akitoa kutoa ushauri wa kitaalamu
kwa kampuni za ndani na nje ya nchi huku akiongoza chama cha NLD akiwa
Mwenyekiti.
Dk Makaidi ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameshaandika zaidi ya vitabu
10. Marehemu ameacha mke aitwaye Modesta Ponela na walibahatika kupata
watoto wanane.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi...Emen!.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni