Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Martha Mlata,
(wa pili kulia), akizungumza na baadhi ya wasanii kwenye viwanja vya
Bunge Mjini Dodoma jana.Picha: Khalfan Said
Semina ya Siku ya Msanii inatarajiwa kufanyika Oktoba 22 na 23 mwaka huu katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere (Makumbusho Posta) na wasanii watafundishwa mambo mbalimbali.Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Adrian Nyangamale, alisema wasanii wanapaswa kujiandikisha kwenye semina hizo ili kupata ujuzi wa mambo mbalimbali.
“Semina hizi ni muhimu kwa sababu kutakuwa na wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali ambao watakuja kutoa mafunzo kwenye semina hizo, jambo ambalo litachangia uelewa na elimu ya wasanii, tumekuwa tukilalamika kuwa hatupati fursa za elimu lakini Siku ya Msanii imetupa hiyo nafasi sasa tuitumie,” alisema.
Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho la Filamu, Selemani Ling’ande alisema wasanii wajitokeze kwenye semina hizo lakini pia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kupiga kura za kupata watu watakaowania tuzo za Siku ya Msanii.
“Semina ni muhimu lakini kuna suala la kutambulika mchango wa wasanii, hapa ndiyo Watanzania wanapotakiwa kufanya mapendekezo yao, kuna fomu zinatolewa kwenye magazeti na mitandao juu ya Tuzo za Humanitarian Award na Life Time Achievement ambazo wasanii wote wanaweza kushindanishwa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Haak Neel Production, Godfrey Katula, ambaye kampuni yake ndiyo imepewa jukumu la kusimamia Siku ya Msanii, alisema Watanzania wajitokeze kupendekeza majina ya wasanii wanaostahili kupata tuzo na Kamati ya Utafiti itakwenda kuhakiki taarifa zote zilizowasilishwa kwao.
“Kazi za wasanii zinaanza kutambulika hapo, wananchi wanawajua hivyo ni fursa yao kuonyesha kuthamini kazi zao, lakini pia tunawataka wasanii wajitokeze kwenye semina ambazo zitafanyika kwa siku mbili ili kupata elimu sahihi,” alisema.
Siku ya Msanii inaandaliwa na Kampuni ya Haak Neel Production kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni