TANGAZA NASI

Breaking

Jumanne, 24 Machi 2015

BI SHAKILA:- KWA SASA HAKUNA TAARAB, KUNA TARADANCE, VIDUKU, BAIKOKO NA KANGA MOJA!.


 NA KAIS MUSSA KAIS
“'Macho yanacheka, moyo unaliaaa, macho yanacheka aeeh, moyo unalia, nikimkumbuka wangu my dear ''
Hayo ni baadhi ya maneno yaliyo katika wimbo aliouimba Bi Shakila alipokuwa na Bendi ya JKT miaka 1980 -1990, ambao ulijizolea umaarufu mkubwa ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.

Mkongwe huyo aliolewa mwaka 1960 alipokuwa na umri wa miaka 11 na mwanamume ambaye alizaa naye mtoto mmoja.

Shakila Said Khamis maarufu kwa jina la Bi Shakira  ni mmoja wa waasisi wa muziki wa Taarabu nchini, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Waimbaji wa Taarabu Tanzania ambacho uhai wake upo kama haupo!.
BI SHAKILA SAIDI KHAMISI.
Katika mahojiano na mtandao huu, Bi Shakila alieleza kuwa alianza kuimba taarabu sambamba na marehemu Saada Binti Saad, mwaka 1960 baada tu ya kuolewa na baadaye moja kwa moja alijiunga katika Bendi ya JKT aliyoitumikia kwa zaidi ya miaka 40.

"Nilianza muziki mwaka 1960 kabla ya Uhuru na nimekuwa huko kwa miaka mingi. Kabla ya kuanza muziki, nilimkuta marehemu Saada Binti Saad, Bi Kidude yeye nilimkuta akiwa tayari amejiunga na ngoma za Unyago, alikuwa bibi yangu na mtu wa karibu sana na mimi wakati huo nilikuwa na miaka sita.”

Hayo ni baadhi ya maelezo ya awali Bi Shakila katika mahojiano na mtandao huu nyumbani kwake mbagala  Charambe jijini Dar es Salaam, kabla ya mfululizo ufuatao wa maswali na majibu na mwandishi wa makala haya.

UBUYU WA TAARAB: Hali yako kiuchumi kwa sasa ikoje?

Bi Shakila: Sina pesa, kiwango ninachokipata kama kiinua mgongo hakinitoshi kabisa. Nalipwa Sh80,000 kwa mwezi na NSSF, matumizi yangu kwa siku ni zaidi ya Sh15,000 kwa siku. Nilistaafu mwaka 2009, lakini mpaka sasa huwa naendelea na kazi yangu pale JKT mara chache na kama tukifanya shoo huwa napewa nauli Sh3000 inayonisaidia kunirudisha nyumbani. Kwa sasa hali yangu ni mbaya kiuchumi.

UBUYU WA TAARAB: Katika kipindi chote cha kazi yako hukuweza kujiwekea vitega uchumi, kama ndivyo sababu ni zipi?

Bi Shakila: Zamani muziki ulikuwa kama starehe, tulilipwa ujira mdogo na hata kukiwa na shoo tulipata ujira mdogo. Kwa sasa muziki ni ajira, tena kubwa kuliko ofisini, lakini umri umeshaenda sana na sisi wakongwe tunatamani haya yangekuwepo hapo nyuma, hii ndiyo sababu ya mimi kushindwa kuweka vitega uchumi.

UBUYU WA TAARAB: Unadhani Serikali inaweza kukusaidia?

Bi Shakila: Kabisa, sisi wakongwe hatuthaminiwi na tunatupwa jalalani, lakini watoto wadogo wavuta unga ndiyo wanasaidiwa, Msanii Ray C alienda mwenyewe kuvuta unga akijua kabisa ni kinyume cha sheria, lakini Serikali imemsaidia, kwa nini na sisi tusiangaliwe?.
UBUYU WA TAARAB: Pole! Wewe huamka saa ngapi na nini majukumu yako ya kutwa nzima?

Bi Shakila: Naamka saa 11 alfajiri kwa ajili ya kuanza kuandaa unga wangu wa vitumbua na maandazi, baada ya hapo naanza kupika. Alhamdulilahi, nina wateja kidogo wanaoniungisha. Saa4 asubuhi namaliza, napumzika kidogo na kuanza kuanza kutengeneza visheti hadi saa 12 jioni. Naoga, napumzika na wanangu tunazungumza mawili matatu kisha naenda kulala hadi kesho tena. Kama ninakwenda mazoezi JKT, basi siku hiyo ratiba yangu huvurugika kidogo. Biashara ya vitumbua nimeifanya kwa miongo minne sasa.

UBUYU WA TAARAB: Kwa kulinganisha na wakati wenu, unadhani taarabu ya sasa inakua?

Bi Shakila: Taarabu kwa sasa hakuna. Kwa sasa kuna rusha roho, taradance, mipasho, kiduku na  khanga moja. Vitu hivi vimevamia na kuiharibu taarabu yetu. Zamani taarabu ilikuwa na ustaarabu na waimbaji tuliimba kwa staha na maneno yalikuwa ya kuburudisha na kusifia kitu fulani si sasa hivi. Hii wanaita Morden Taarabu na wengine taradance sijui nini mimi siikubali kabisa.

UBUYU WA TAARAB: Maisha yako ya ndoa yalikuwaje?

Bi Shakila: Niliozwa nilipokuwa na miaka 11. Mume aliyenioa kwa ndoa aliniacha mwaka mmoja baadaye kwa kuwa tulitofautiana kwa mengi. Aliniacha nikiwa na mtoto mmoja mchanga, hapo ndipo nilipoanza balaa hilo. Niliolewa tena na mume mwingine huyu niliishi naye miaka 18 na kuzaa naye watoto watano, mwaka 1975 alifariki, iliniuma sana nikakaa eda.
Baadaye niliolewa na mume mwingine, huyu nikazaa naye watoto watano na baadaye tuliachana. Nikaolewa tena kwa mara ya nne, nikazaa watoto wawili, nilipokuwa na mimba ya huyu mtoto wa mwisho mwaka 1993, mume akaniacha. Mwanangu wa mwisho Shani nilimzaa Ijumaa ya tarehe 27 Machi 1993. Tangu hapo niliwachukia wanaume na sijataka kuolewa tena mpaka leo.

UBUYU WA TAARAB: Waimbaji wa muziki wa taarabu waume kwa wanawake huoa sana au kuolewa na kuachika, tatizo ni nini?

Bi Shakila: Sijui, kwa kweli mimi siyo kwamba nilikuwa nikiacha wanaume, hapana ila walikuwa wakiniacha wao. Kwa upande wangu nahisi ilitokana na kuwa mwanamuziki na wakati huo muziki ulichukuliwa kama uhuni. Lakini huenda kuna sababu nyingine ambazo mimi sizijui..

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni