TANGAZA NASI

Breaking

Jumatatu, 21 Machi 2016

BARUA YA WAZI KWA KAMATI YA MAANDALIZI YA SHINDANO LA KILIMANJARO MUSIC AWARD'S 2016.

NA KAIS MUSSA KAIS.
   "0657 - 036 328".


           Asalaam aleykum wasomaji wa mtandao huu wa ubuyu wa taarab tanzania, leo tumekutana tena katika kona hii maalum ambayo tumekuwa tukiabarishana mambo kadha wa kadha kama ilivyo ada yetu!.

 

    Nimeamua nizungumze na ndugu zangu, kaka zangu, baba zangu kamati nzima ya shindano la kilimanjaro music awards ambalo hufanyika mara moja tu kila mwaka, kwanza kabla ya yote nawapongeza sana kwa shindano lenu kwani limekuwa likijizolea umaarufu takribani kila mwaka, pongezi zaidi ziende kwa mbunifu mkuu wa tukio hili. pamoja na yote hayo lakini kumekuwa na mapungufu kidogo katika vipengele vyenu hususani huu upande wa muziki wa taarab nchini tanzania.

 

    1. Wajumbe ambao mmekuwa mkiwaita kuja kuizungumzia taarab kila mwaka sura zimekuwa ni zile zile tu wala hazibadiliki, na hata kama msipobadilisha lakini kwa kuwa mmeamua hawa watangazaji wa muziki huu wa taarab ndio waje kupendekeza nyimbo ambazo zimekuwa zikifanya vizuri redioni, mngeangalia na mikoani napo kwani redio ambazo zina vipindi vya taarab zipo na zimekuwa zikipiga nyimbo hizo, sio mbaya hata mwaka huu mkajaribu kuchanganya wajumbe hao ili kuleta challenge zaidi.

 

   2.Kwa wenzetu wa muziki wa bongo fleva mmeweka kipengele cha msanii anae chipukia ambapo mwaka jana alishinda Baraka the prince!, lakini kwa upande wa huku kwetu taarab hakuna kipengele kama hicho ina maana hamuoni kama kuna umuhimu huo?, au hakuna waimbaji wachanga wanaochipukia mkaonyesha ni kwa kiasi gani mnawathamini kwa kuwawekea kipengele chao?. mwaka jana mmemchukua muimbaji mchanga ambae alifanya vizuri Fatma nyoro wa jahazi modern taarab mkamuweka na wakongwe khadija kopa na isha mashauzi hapo mnatarajia anaweza kushinda mbele ya wakongwe hao?, pale hamkuwa sawa na mlimpotezea nafasi yake ya kushinda tu waziwazi, tunaomba kipengele cha msanii anaechipukia kiwepo mwaka huu ili kuwapa hamasa zaidi wasanii wachanga hapa nchini.

 

  3.Kuna wasanii wakongwe ambao waliifikisha hapa ilipo taarab mpaka mimi na wewe tukaitambua na kuipenda lakini kwa sasa hawajihusishi kabisa na muziki huu au wengine wametangulia mbele ya haki, hawa kwanini msiwaandalie zawadi maalum ya heshima kama ambavyo mmekuwa mkifanya katika dansi kwa kuwapa hadhi hiyo akina marehemu mzee ngurumo na wengineo?, taarab ni muziki wenye historia kubwa sana juu ya uhuru wa nchi yetu ya tanzania, jaribuni kuwajari na kuwathamini hawa wazee wetu basi japo kwa tuzo.

 

  4.Kuna hiki kipengele cha wimbo bora wa mwaka, kwanini mmekuwa mkichanganya miziki yote katika kipengele kimoja?, ushauri wangu hiki kipengele kinatakiwa kufanyiwa mabadiliko, kila aina ya muziki ujitegemee na sio kuchanganya kama mfanyavyo sasa.

 

  5.Kule visiwani unguja kuna bendi nyingi sana zimekuwa zikipiga taarab asilia mpaka hapa dar zipo pia baadhi ya bendi kama hizo, lakini kwa nini hamkuweka kipengele cha tuzo zinazohusu taarab asilia? na hizo bendi zina nyimbo zao mpya na zinachezwa katika redio mbalimbali, lile shindano la wenzetu kule unguja wameweka tuzo ya muziki wa taarab asilia kila mwaka, nionavyo mimi ipo haja kuongeza hiki kipengele ili kuwapa hamasa waimbaji hawa kwani taarab asilia imekuwa ikirudi tena kwa kasi kubwa hapa nchini.

 

       Mwisho kabisa napenda niwatakie maandalizi mema ya mchakato huu kwa mwaka 2016, ila kubwa zaidi naomba myafanyie kazi haya niliyoyazungumza hapa kwani yana umuhimu mkubwa sana na ndio kilio kwa wasanii ambao mmekuwa mkiwashindanisha kila mwaka, naweka kalamu yangu chini tukutane tena wiki ijayo ahsanteni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni