Ile segment yetu pendwa ya kikaangoni wiki hii iliendelea na tulimbambanisha hashim said au mzee wa majanga kutoka mashauzi classic, aliingia katika group saa moja na dakika kumi na maswali yakaanza moja kwa moja, mtangazaji aliepata bahati ya kuanza kuuliza swali alikuwa ni:-
ASHA VICTORIA FM MUSOMA:- Hashim karibu sana humu jandoni kwetu, ningependa kujua historia yako kimuziki na umeshafanya kazi bendi ngapi mpaka sasa na nini sababu ya kuhama hama kwako?.
HASHIM SAID:- Mimi nimeanza kuimba tokea mwaka 1998 na bendi yangu ya kwanza inaitwa kimara connection bendi ambayo ilikuwa inapiga miduara na mchanganyiko wa dansi, baada ya hapo nikapenda kuimba taarab na bendi yangu ya kwanza katika taarab ilikuwa ni all star's iliyokuwa chini ya sabahah muchacho na mumewe salum abdul, baadae nilijiunga na egpytion music club iliyokuwa mtaa wa swahili kariakoo, baada ya pale nilijiunga na babloom chini yake seif kisauji na nilikaa kwa miaka mitano kisha mwaka 2004 nikajiunga na east african melody ambapo nilidumu kwa miaka minne kabla kuchukuliwa na dar modern taarab, lakini baadae nilirudi tena east african melody lakini ilipoanzishwa mashauzi classic nilikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa bendi hiyo na nilidumu kwa miaka minne nikahama na kujiunga na wakaliwao ambapo nilidumu kwa miezi tisa tu, na hapa juzi tu nikaamua kurudi nyumbani yaani mashauzi classic, kuhama hama issue inakuwa maslahi tu na wala sio kitu kingine.
MC CHINGA DODOMA FM:- Hashim kuna tetesi kuwa unataka kurejea bendi yako ya zamani mashauzi classic je kuna ukweli wowote juu ya taarifa hizi?.
HASHIM SAID:- Mc chinga nakupata sana ni kweli nimerudi mashauzi classic na siku alhamisi tarehe 19/5/2016 pale mango garden kuna bonge la party la kunikaribisha rasmi katika ule usiku wa nyumbani ni nyumbani.
SALMA MAISHA FM DODOMA:- Hashim kwanini umeamua kurudi mashauzi na sio bendi ingine nikimaanisha east african melody au dar modern maana mwenyewe unasema huko kote ni nyumbani kwako?, na tangu uanze muziki huu ni mafanikio gani umepata?.
HASHIM SAID:- Salma au kim nainai ni kwamba mafanikio niliyopata katika muziki nashukuru sasa hivi nina kibanda changu nakaa na watoto wangu pamoja na mke wangu nimetoka katika yale maisha ya kupangapanga maana majumba siku hizi kila kukicha yanapandishwa kodi, na kurudi kwangu mashauzi ni sababu niliishi vizuri sana na wenzangu pale kwahiyo kuna vitu nilikuwa navimiss sana kiukweli, ila kwa sasa nashukuru nimerudi nyumbani sasa.
SHUFAA KAYA FM BAGAMOYO:- Katika tasnia ya taarab inasadikika kwa asilimia kubwa kwamba kumejaa rushwa ya ngono je wewe kama msanii wa taarab nchini unalizungumziaje jambo hili?.
HASHIM SAID:- Hata mimi nimekuwa nikisikia kuwa huku kwetu rushwa ya ngono ipo ila sijarithibitisha hilo, ila kwa upande wangu nimewasaidia sana waimbaji wengi na wengine wapo mashauzi mpaka sasa mfano zuhura, rahma na aziza hawa ndio nimewasaidia kuwepo pale mashauzi na sijawahi kuwataka rushwa ya ngono
BLANDINA TK FM TANGA:- Hashim said, mimi swali langu fupi tu ndugu yangu, ni kwanini uliondoka wakaliwa modern taradance?.
HASHIM SAID:- Nimeondoka wakaliwao modern taradance kutokana na kuna vitu vimenifanya mimi niondoke wakaliwao kwanza ucheleweshaji wa nyimbo yangu kupelekwa redio tumeurekodi tokea mwezi wa kumi na moja mwaka jana lakini umekuja kupelekwa redio mwezi wa nne mwaka huu jambo ambalo limenirostisha mimi kama mimi kisanaa, jambo la pili niliamua tu mimi mwenyewe kuachana na wakaliwao sababu nikiangalia heshima yangu mimi pale wakaliwao sikuwa napendeza na nikagundua kuwa nilikuwa napendeza zaidi mashauzi classic na kwakuwa sikuondoka vibaya basi nimeamua kurejea nyumbani na wakaliwao sijaondoka vibaya ingawa kitendo cha kuchelesha nyimbo yangu kiliniumiza sana ila nimepotezea tu ukweli ndio huo!.
KAKA ZEMA CITIZEN NAIROBI KENYA:- Hebu weka wazi maisha yako ya ndoa ulioa ukataliki...kisha ukaoa tena ukataliki...ukaoa tena ukataliki...ukaamua kumrejea mama watoto wako yaani mzazi mwenzio, je ni wanawake wana tatizo au tatizo unalo wewe mbona kusuasua kwenye ndoa kaka?.
HASHIM SAID:- Kaka zema ni kwamba hili ni tatizo kubwa ambalo ninalo katika maisha yangu ya mahusiano, siwezi kujua kama tatizo lipo kwa upande wangu au wanawake ninao waoa, lakini mwisho wa siku ni kwamba nimerejea katika ndoa yangu ya awali kwa mke wangu ambae ana watoto wangu, mimi na yeye tulitengana kwasababu ya maneno ya watu walikuwa wakimlisha maneno kila siku mumoe malaya, mumeo sijui hivi mumeo sijui vile lakini katika maisha yetu ya ndoa hakuwahi kunifumania hata mara moja na talaka aliidai yeye mwenyewe, baadae nikaoa mke wa pili, mke huyu alikuwa akini-cheat yeye alikuwa akifanya kazi za sanaa kwani alikuwa ni mcheza show na nilimuachia huru tu nikijua sanaa sio uhuni lakini alikuwa akitumia nafasi hiyo kuni-cheat sana sana nikaamua kumtaliki. nikapata mke wa tatu fatuma fundikila nilimpenda sana katika wanawake niliowapenda alipata bahati ya kuuteka moyo wangu fatuma fundikila na tumedumu katika ndoa miaka mitatu na sababu kubwa ya mimi na yeye kuachana ni maneno ya familia kwanini anaishi na mimi mwanaume maskini, mwanaume muimba taarab mwanaume mwenye kipato cha chini maneno yalizidi mwisho wa siku miluzi mingi humpoteza mbwa! mwisho wa siku tuliachana na nilimuacha huku nikiwa bado nampenda sana!.
TNNA EBONY FM IRINGA:- Nafahamu ulikuwa na bibie Diana kwenye mahusiano lakini sasa yamefikia mwisho lakini mbona diana anakusumbua sana kiasi cha kusema katika redio flani kwamba yupo tayari umrejee hata leo kwani nini kubwa mno ulilokuwa unamfanyia mpaka anaonekana kuumia na penzi lako mpaka anataka umrejee?.
HASHIM SAID:- Diana ananipenda mpaka sasa hilo nalijua wazi ila tabia zake zimenishinda, sasa hivi nasikia yupo na mtu anaishi nae lakini kila siku haishi kunipigia simu na kuniambia kuwa bado ananihitaji, najua ni ngumu kunisahau yeye maana nilikuwa namfanyia vitu vingi vizuri vya mapenzi, nilikuwa namfulia, nilikuwa nampikia, nilikuwa namkata kucha akitaka kulala ni lazima nimlaze kifuani kwangu ndio apate usingizi na mambo mengi mazuri na matamu kwenye mapenzi hivyo ni ngumu sana kunisahau mtu kama mimi.
Maswali yalikuwa mengi sana toka kwa watangazaji mbalimbali lakini siwezi kuorodhesha maswali yote hapa kutokana na nafasi na muda pia ila baadhi yao niwataje kwa majina tu ni Aisha wa barmed's televisheni mwanza, aisha saggaf wa k.b.c. nairobi, nadya wa bomba fm znz, malick wa hits fm znz, koleta wa redio free mwanza, edna wa afm dodoma, kitoroli wa mlimani redio dar, mamaa madikodiko wa pilipili fm mombasa, hamida malick wa coconut fm znz, mamaa nyeupe wa upland's redio njombe, asha simba wa kilosa fm morogoro, fortina wa cg fm tabora na wengineo wengi. tukutane tena wiki ijayo...Ahsanteni sana!.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni