TANGAZA NASI

Breaking

Jumapili, 12 Aprili 2015

VITUO VYA REDIO NA TELEVISHENI, WAANGALIENI WASANII WA TAARAB HIVI THAMANI YAO KWENU NI IPI?.

Wapenzi wasomaji wangu leo nipo katika ule muendelezo wa kuwaletea mambo mazuri toka kwangu, na jumapili ya leo tupo na kile kipengele chetu kipya kabisa cha makala ya wiki ambayo itakuwa ikikujia kila siku ya jumapili hapa hapa katika Blog yako bora ya taarab nchini tanzania ya ubuyuwataarabutz.blogspot.com

 

   Taarab ni muziki wenye asili ya pwani, haswa ya mashariki ijapokuwa kwa sasa muziki huu umejipatia umaarufu na kusambaa karibia nchi nzima na hata ile mikoa ya nyanda za juu kusini nazungumzia mikoa ya mbeya, iringa na kwingineko taarab imekuwa ikifanya vizuri sana. Kikubwa kinachonisikitisha na kunishangaza ni maisha duni ambayo wamekuwa wakiishi wasanii wa fani hii huku wamiliki wa vituo vya redio na televisheni wakijipatia wadhamini katika vipindi vya taarab na kuendesha vyema maisha yao na wafanyakazi wao kwa ujumla.

 

Wewe kama mdau hebu jaribu kufanya tasmini yako tu, na hii haitakiwi mtu awe na elimu kubwa ili kuweza kung'amua ukweli halisi ninao umaanisha hapa! karibia vituo vyote vya redio na televisheni vimekuwa na vipindi vya muziki huu wa taarab tena wakivipa vipindi hivi masaa matatu na zaidi ya "air time" huku vikiwa na wadhamini lukuki ambao wamekuwa wakivilipa vituo hivyo mamilioni ya pesa, lakini cha kujiuliza hawa wahusika haswa wa muziki huu nikimaanisha wavuja jasho wenyewe wanamuziki wananufaika vipi na udhamini huu wa makampuni katika kazi zao ambazo wamekuwa wakiziandaa kwa mazingira magumu?.

 

Ukipata bahati ya kutembelea katika bendi yoyote ambayo inaandaa nyimbo zake mpya utaamini haya niyasemayo, wanakuwa katika hali ngumu sana, chakula cha mchana wakati wa mazoezi husika  wanakula kwa shida, nauli ya kuwarudisha majumbani baada ya mazoezi nayo ni tabu, siku wanayokwenda kurekodi utawaonea huruma wanashinda studio kuanzia asubuhi mpaka jioni! wakitoka hapo wamechoka hoi wanarudi nyumbani, lakini nyimbo zikishapelekwa katika media mbalimbali watu wanakula kiulaini kupitia kazi zao, hali hii itaisha lini? thamani haswa ya mwanamuziki wa taarab ipo wapi?.

 

labda nishauri jambo moja kwa wamiliki wa vituo vya redio na televisheni ambao wamekuwa wakinufaika kwa namna moja ama ingine na kazi hizi za wasanii wa taarab nchini, wakati wakisubiri sheria itungwe bungeni juu ya haki za wasanii na vituo vya redio na televisheni nchini, waandae utaratibu wa kurudisha shukrani au kifuta jasho kwa bendi za taarab na wasanii kwa ujumla, hususani wale ambao wamekuwa wakimenyeka kila kukicha kuandaa nyimbo mpya ambazo wamekuwa wakizitumia kwenye vipindi vyao. wanaweza kuwasaidia kwa style yoyote ile wanayoiona wao inafaa ili kuwapa motisha na nguvu ya kufanya mambo mazuri zaidi ya hapo kwa ajili yao na wananchi kwa ujumla.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni