TANGAZA NASI

Breaking

Jumatatu, 15 Juni 2015

MALIK SHAKHRAN WA HITS FM 92.5:- WATANGAZAJI TUACHE KUBAGUA BENDI NA NYIMBO ZA KUCHEZA REDIONI


NA KAIS MUSSA KAIS.

            Habari za jumatatu hii wapendwa wasomaji wangu wa ubuyuwataarabutz.blogspot.com, leo ni siku ingine tena tunakutana katika hiki kipengele chetu cha mjue mtangazaji wako kama ilivyo ada!, na leo tupo na mtangazaji Malik Shakhran wa "Hits redio 92.5 fm" redio hii ipo visiwani zanzibar na kipindi anachokiendesha kinaitwa "msisimko wa pwani" ambacho kipo kila siku ya jumatatu mpaka ijumaa kuanzia saa saba na nusu mpaka saa kumi kamili jioni.


      Nilianza kwa kumuuliza historia yake kwa ujumla ipo vipi wadau na wapenzi wake wangependa kujua na kumfahamu zaidi, nae alianza kwa kusema kwa jina naitwa Malik Shakhran ni mtoto wa mzeeSaid Shakhran Mwangia, ambae kwa sasa ni marehemu mwenyezimungu amrehemu Baba yangu kipenzi, mimi ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto saba wa familia yetu wanaume tupo watatu na wanawake wapo wanne.


MALIK SHAKHRAN AKIWA KATIKA KIPINDI NDANI YA HITS FM 92.5

    Nimezaliwa mnamo mwaka 1980 hapo hapo Dar, na nikasoma mnazi mmoja primary school mpaka darasa la saba kisha nikaja huku zanzibar kwa wazee wangu nako nikasoma mpaka kidato cha sita, baada ya hapo nikaenda kusomea ualimu, nilipomaliza ualimu nikaona ni vyema nikasomee uandishi wa habari fani ambayo naipenda toka moyoni. Nikaenda kusomea uandishi wa habari hapa zanzibar katika chuo cha habari nikahitimu mwaka 2009.


  Baada ya kumaliza tu nikaja hapa Hits fm moja kwa moja, hivyo naweza kusema kuwa hapa Hits fm ni sehemu yangu ya kwanza kufanya kazi na ndipo nilipo mpaka sasa na mpaka sasa nina miaka sita bado nipo hapa hapa. nimejaaliwa kuoa mwaka 2013 na namshukuru mungu nimejaaliwa kupata mtoto mmoja aitwae "Shymaa" nampenda sana.


UBUYU WA TAARAB:- Ukiwa kama mdau na mtangazaji wa taarab, unauzungumziaje muziki huu kwa takribani miaka hii mitano ya mabadiliko?.


MALIK SHAKHRAN AKIWA NA KHADIJA OMARY KOPA NDANI OFISI ZA HITS FM.

MALIK SHAKHRAN:- Kiukweli taarab halisi haswa katika miaka hii inakufa tena inateketea kwa mengi sana, washairi wamekuwa hawatungi mashairi yenye kuleta mafunzo mazuri kwa jamii kama ilivyokuwa zamani hatupati zile tamithali za semi na misemo yenye maana matokeo yake wamejikita kwenye malumbano yasiyo na tija hususani katika taarab ya sasa, chamsingi watunzi wanatakiwa wabadilike na watumie lugha yetu ya kiswahili katika kudumisha mila na desturi zetu kama zamani waache kuleta hadithi za mwamba ngoma.


UBUYU WA TAARAB:- Kumekuwa na malalamiko toka kwa wamiliki wa vikundi vya taarab na wasanii kwa ujumla, wengi wao wanasema ninyi watangazaji mmekuwa na kasumba ya kucheza nyimbo za bendi kubwa kubwa na zenye majina na bendi zingine zikikosa "air time" hili unalizungumziaje?.


MALIK SHAKHRAN:- Daah! nasikitika sana katika hili ndugu mwandishi, kwa wale watangazaji wenye tabia kama hizi za kubagua mabendi na wasanii nawaomba waache kwani sio jambo zuri hata kama msanii kakukera mambo yenu ya nje msiyatie katika kazi, tatizo watu wanaendekeza umimi na ushoga katika kazi na ukishayaingiza mambo hayo katika kazi basi umeshaharibu, nawaasa waache!.


UBUYU WA TAARAB:- Una ushauri gani kwa wasanii na wamiliki wa bendi za taarab hapa nchini?.


MALIK SHAKHRAN:- Cha kwanza viongozi wa mabendi na wasanii walete ushirikiano na umoja ili kudumisha muziki huu wa taarab, maana kwa upande wa taarab ushirikiano ni mdogo sana kwa kila jambo na sio kwenye raha tu bali mpaka shida ushirikiano ndio kila kitu...tuondoshe chuki hasama na husda!.


UBUYU WA TAARAB:- Mwisho ni mtangazaji gani wa kipindi cha taarab ambae anakuvutia sana kwa kazi zake pindi anapokuwa redioni?.


MALIK SHAKHRAN:- Nawapenda wote takribani, ila "Sauda Mkalokota" wa zenji fm nampenda sana sababu ametulia katika utangazaji wake na hana papara mungu amuongoze zaidi ili aweze kufika mbali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni