Alianza kupenda soka akiwa kijana mdogo, ndoto zake za awali zilikuwa
kucheza soka, baadaye zikageuka na kujikuta akimbo taarabu. Wakati huo,
Tego alikuwa na mazoea ya kufuatana na baba yake kwenye mazoezi na
maonyesho ya kundi lililowahi kutamba la muziki wa taarab asilia la
African Musical Club. Tego anasema alilazimika kubadili mipango yake
kutokana na kuvutiwa na aliyekuwa muimbaji nyota wa taarab nchini na
katika ukanda nzima wa Afrika Mashariki na Kati, marehemu Issa Matona
aliyekuwa akiliimbia kundi hilo pamoja na baba yake.
Anasema, "kwa kweli sikuwaza kuja kuwa mwanamuziki, ndoto zangu
zilikuwa ni kuwa mchezaji wa soka, lakini kumshuhudia na kumsikia
marehemu Issa Matona nilijikuta nabadilisha mawazo na kuanza kujifunza
muziki kupitia kundi hilo la Africa Musical Club mwaka 1995," Tego
anasema kabla ya kupenda muziki kupitia kwa baba yake, aliyekuwa
muimbaji na kiongozi wa kundi la African, alikuwa 'kichaa' wa soka,
akianza kucheza timu ya Santos ya Mtoni alipokuwa akiidakia kabla ya
kucheza nafasi za mbele baadaye.
Anasema, "nilianza kucheza soka tangu nikiwa Shule ya Msingi Sokoine
na timu yangu ya mtaani ilikuwa ni Santos niliyokuwa nashiriki nayo
kwenye michuano ya Yosso kama golikipa, kabla ya kuvutwa na marehemu
baba yangu kuingia kwenye muziki kwa kuhudhuria mazoezi ya kundi lao."
Anasema alianza muziki kwa kujifunza kupiga ala mbalimbali kabla
yakujikita kwenye utunzi na uimbaji akiwa katika kundi hilo la African
hadi baba yake alipohama na kuanzisha kundi lake binafsi la Coast Modern
Taarab mwaka 1998 ambapo alizidi kubobea kwenye fani hiyo.
Tego anasema mwaka 2003, aliliacha kundi hilo la baba yake na kwenda
Zanzibar kujiunga na kundi la JKU, lakini alilazimika kurejea jijini Dar
es Salaam miaka miwili baada ya baba yake kufariki na baada ya mazishi
alilazimika kubeba jukumu la kuliongoza kundi hilo. "Nilirejea Dar mwaka
2005 baada ya baba kufariki na nikabeba jukumu la kuliongoza kundi hilo
ambapo tangu liwe chini yangu tumeachia albamu tatu tofauti, ya kwanza
ikiwa ni I'm Crazy 4 U', 'Kupenda Isiwe Tabu' na 'Damu Nzito' ambayo
inaendelea kutamba kwa sasa," anasema.
Tego anasema fani ya muziki imempa mafanikio mengi ikiwemo kujenga
nyumba anayoishi na familia yake, kumiliki gari, kuwasomesha na
kuwalisha wanae wanne pamoja na kumiliki miradi mingine ya kibiashara
ambayo hakupenda yaanikwe gazetini. Mkali huyo, anayefananishwa na Mzee
Yusuph wa Jahazi Modern, kwa namna ya madoido yake ya uimbaji, alisema
hakuna kinachomuuma kama wizi wa kazi za wasanii unafanyika nchini,
akidai kama angekutana na Rais wa Tanzania, hilo ndio lingekuwa kilio
cha kwanza kwake.
"Ningemuomba Rais atusaidie kushughulikia wizi wa kazi zetu,
tunaibiwa sana, licha ya kuwepo kwa COSOTA na asasi nyingine za
kukomesha vitendo hivyo, ila kama mie ningekuwa Rais wa nchi ningepigana
kuinua maisha ya wananchi pamoja na kuipa kipaumbele michezo na sanaa
kwa sababu ni njia nzuri ya kutatua tatizo la ajira nchini," anasema
Tego.
Tego, anayeshabikia klabu ya Yanga na Arsenal ya Uingereza, alisema
hakuna tukio la furaha kwake kama kukubalika kwa kazi yake ya 'I'm Crazy
For You', iliyoliinua Coast Modern na kuzalisha albamu iliyobeba jina
hilo iliyomweka kwenye ramani ya muziki wa taarab nchini. Nyota huyo,
aliyeoana na Fatuma Mohammed aliyezaa naye watoto wanne, Said , Ikram,
Khairat na Ashura anapendelea wali kwa samaki na kinywaji anachopenda
kukitumia baada ya chakula ni juisi.
Tego, mwenye ndoto za kuwa mwanamuziki wa kimataifa kwa kuitangaza
taarab nje ya mipaka ya Afrika, alisema pamoja na kuimba taarab,
anavutiwa sana na Jose Mara wa FM Academia na Christian Bella wa malaika bendi. Huyo ndie omary tego the special one ukipenda muite mgodi unaotembea mkurugenzi wa coast modern taarab yenye makazi yake jijini dar!.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni