NA KAIS MUSSA KAIS
+255657036328
Mohammed Ilyas ni muimbaji maarufu ambaye anajulikana kama Professa
wa muziki wa taarab ya asili ambaye amezaliwa katika Mtaa wa Vikokotoni
Mjini Zanzibar mwaka 1942 na kupata elimu yake ya msingi skuli ya
Darajani hadi darasa la nane.
Professa Ilyas wakati akiwa shule ya msingi alianza kujifunza kuimba
nyimbo mbali mbali ambapo alikuwa akimuhusudu sana mwalimu wake ambaye
kwa sasa ni marehemu Seif Salim aliyekuwa muimbaji wa kikundi cha Taarab
cha Malindi (Malindi Musical Club) .
Maalim Seif Salim alikuwa muimbaji na mtungaji wa nyimbo mbali mbali
za taarab katika kikundu cha cha mwanzo hapa zanzibar cha Akhawan Safaa
ambapo kikundi hicho kilianzishwa mwaka 1905 na amewahi kupata zawadi
kadhaa katika medani hiyo ikiwemo ile ya Bill Board Award ya Nchini
Marekani.
Mnamo mwaka 1964 Ilyas aliacha kuendela na masomo yake na badala yake
alianza kujifunza rasmi kuimba huku akimfuata mwalimu wake katika
kikundi hicho ambacho kinajulikana zaidi kwa jina la ngudu wa Akhwan
Safaa (ndugu wapendanao).
Wakati huo Ilyas alikuwa na umri wa miaka 14 alianza kuimba akianzia
na nyimbo za kiserikali ambazo zilikuwa zikiyasifu mapinduzi
yaliofanyika mwaka 1964 ambapo yaliung’oa utawala wa kisultani.
Ilyas alisema wakati huo alikuwa na wenzake akina Abdallah Issa,
Mukrim na Mohammed Seif Khatib ambaye sasa ni Waziri wa Habari Utamaduni
na Michezo Tanzania Bara.
Alisema alianzia na kupiga filimbi (nai) na kifaa kimoja cha kuleta
sauti ambacho hujulikana kwa jina la (flut) huku akipata nafasi ya
kuimba nyimbo moja moja kwa vile mwanafunzi alikuwa akimfuata sana
mwalimu wake katika uimbaji.
Mnamo mwaka 1968 Ilyas alianza kutunga nyimbo ambayo ikiitwa
‘Nimeumbika’ ambayo aliitia muziki mwenyewe na kutungwa na Mwalimu wake
Maalim Seif Salim.
Ilyas alisema wakati mwengine akawa anatunga nyimbo na kuimbwa na
Mwalimu wake Seif Salim huku yeye mwenyewe akiitia muziki kama nyimbo ya
‘Shaka’.
Mwaka 1969 Ilyas alianza kupanda chati kidogo kidogo kutokana na
uimbaji wake katika majukwaa ambapo sauti yake ilikuwa ikiwavutia watu
wengi wanaofika katika ukumbi kusikiliza taarab.
Zanzibar miaka hiyo hakukuwa na mambo ya starehe kama yaliopo hivi
sasa ambapo watu wengi walikuwa hawana pa kwenda zaidi ya kwenda kwenye
kumbi za taarab kutokana na vikundi vikundi viwili pekee ndio vilivyokuw
amaarufu ukiacha hicho cha Malindu chengine ni Culture Musical Club
ambacho ni cha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
1970 Professa Ilyas baadae aliamua kwenda Dar es salaam kutokana na
hali ya kimaisha na kujiunga na kikundi chengine cha taarab cha Alwatan
ambapo huko alikutana na waimbaji wengine kama Abdulhalim Attas,
Abdallah Awadh na Said Awadh na wengine katika kikundi hicho ambao pia
nao walipata mafunzo katika kikundi cha Malindi.
Mohammed Ilyas aliendelea kuimba na kikundi cha Awatan hadi mwaka
1972 ambapo alipata nafasi ya kwenda Mkoa wa Shinyanga kwa uwenyeji wa
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Mustapha Songambele ambapo alipata kuanzisha
kikundi kipya mkoani huko kikiitwa Shinyanga Musical Club.
Ilyas alisema yeye alikuwa ni mwalimu wa kikundi hicho ambapo alipata
wanafunzi wengi wa kujifunza kuimba nyimbo za taarab pamoja na kutunga
mashairi.
Baadae Professa Ilyas alirudi tena Zanzibar mwaka 1980 na kurejea
katika kikundi chake cha asili cha Akhwan Safaa na kuendelea na kupiga
muziki huku akiwa ameshapata uzoefu wa kutosha katika kutunga mashairi
ya nyimbo, kutia muziki na kupiga vyombo mbali mbali vya muziki huo.
Wakati huo ndipo alipopata kutunga nyimbo ikiwemo Usijigambe, Khofu
yako ondoa na Nisafirishe kwa huba huku nyimbo yake maarufu ambayo
ilimpatia umarufu mkubwa visiwani hapa na nje ya nchi iitwayo ‘Pendo
lawasikitisha’.
“Nyimbo iliyonipa umaarufu mkubwa ni Pendo lawasikitisha na ndio
ninayoipenda sana ingawa nyimbo nyingi zimenipa umaarufu lakini hii ndio
khasa” alisema.
Mohammed Ilyas alifunga ndoa na Bi Maryam Hamdan mwaka 1985 na baadae
walisafiri pamoja kwenda Ujerumani ambapo Bi Maryam alikwenda kwa
masomo na huko walipata nafasi ya kujifunza mambo mengi ya muziki baada
ya kukutana na mwalimu mmoja wa chuo cha muziki Professa Helmut Grab na
kuwataka kutengeneza muziki kitaalamu ikiwa pamoja na kutunga katika
njia fasaha, kuweka style za kisasa na ku control pumzi wakati wa
kuimba.
Wakati akiwa Ujerumani ghafla alikutana bila ya kutarajia na mjumbe
wa kampuni ya Kiingereza iitwayo ACE Recording na kumtaka kurikodi
nyimbo za taarab mbali mbali za visiwani Zanzibar.
“ Mie sio mchoyo na ndio nilipopata huyu mjumbe wa kampuni ya ACE
nilirudi naye Unguja na kuja kurikodi vikundi mbali mbali ili na
wenzangu wapate kunufaika sio nitajike mie peke yangu kw ahivyo
tulirikodi nyimbao nyingi katika vikundi vingi mpaka kidumbak” alisema
Professa Ilyas.
Alisema aliporudi Zanzibar alirikodi nyimbo zake na nyengine za
vikundi vyengine ikiwemo kikunci cha Culture Musical Club, Royal Air
Force, Sahib l –aar, Kidumbak na nvyenginevyo ili navyo vipate umaarufu
duniani.
Alisema kuanzia hapo Zanzibar ikaanza kufahamika ndani na nje ya nchi
kutokana na uimbaji wake wa taarab vikundi vyengine ambavyo ni vya
mitaani vikaanza kufifia kidogo kidogo na hatimae kufa kabisa.
Mnamo mwaka 1989 Ilyas alijipumzisha kwenda katika kikundi chake
maarufu cha Akhwana Safaa na akaamua kuanzisha kikundi chake kiitwacho
Tinkle Star Modern ambacho kilikuwa kikipiga muziki kwa kutumia vifaa
vya kisasa hapo tena ndipo Bi Maryam mke wa Professa alipoanza kumtafuta
Bi Kidude na kuanza kuimba naye ili katika kikundi hicho.
Professa alisema walianza kumtangaza Bi Kidude na kusafiri naye
kwenda nchi za nje ambapo walikwenda kupiga taarab katika nchi kadhaa
duniani ikiwemo Ufaransa, Uingereza, Japan, Italy Finland, Dubai, Oman
na Ujerumani.
Alisema kwamba kinachomfurahisha ni kuona bado wananchi wengi wa
visiwa vya Zanzibar bado wanazipenda nyimbo zake na kupenda taarab ya
asili licha ya kuzuka vikundi vingi vya taarab ambavyo aliviita visivyo
na muelekeo.
Gwiji huyo wa taarab alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado
haijaithamini fani ya muziki visiwani hapa kutokana na baadhi ya
viongozi kutoshughulikia sanaa hiyo.
Alisema la kushangaza serikali ilitakiwa iwe ya mwanzo kuthamini
wasanii wake lakini imekuwa ikiwapuuza hata pale wanapostahiki kusaidiwa
nayo hushindwa kufanya hivyo jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo
wasanii wengi ambao wamejitolea kwa hali na mali katika kuinua sanaa
hiyo ya muziki wa taarab.
Alisema wasanii wengi walikuwa wakitumika katika kuimba nyimbo mbali
mbali za kuhamasisha nchi kuwa na amani lakini bado serikali haijaona
umuhimu wa jambo hilo.
Alisema mwaka 1994 wakati Dk. Salmin Amour Juma akiwa Rais wa
Zanzibar wasanii waliitwa Ikulu kupewa zawadi na vyeti vya usanii bora
lakini kutokana na kushiriki Tamasha la Mzanzibari ambalo lilianzishwa na Rais kwa lengo la kuuenzi utamaduni wa Zanzibar.
Lakini kutokana na urasimu wa watendaji wa SMZ, Professa Ilyas
alisema walipewa vyeti pekee kwa kuwa vilitolewa mbele ya Rais lakini
zawadi ambazo zilikuwa na fedha kadhaa hawakupewa kabisa jambo ambalo
halikuonesha sura nzuri katika jamii ya wasanii.
“Sina haja ya kumtaja jina aliyezuwia zawadi zetu ambazo ni fedha
zilizotolewa kwetu lakini tunajua aliyechukua fedha zetu kwa sababu yeye
alikuwa na nafasi hapo Ikulu atatumia miaka mingapi?” alihoji.
Alisema wakati wa kampeni alitunga shairi moja la kuhamasisha amani
na utulivu na kulitia muziki yeye mwenyewe na baadae alikwenda kwa
gaharama zake kurekodi katika studio za Televisheni Zanzibar (TVZ) na
Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) ili zipigwe nyimbo hizo.
Alisema nyimbo hizo huwa zinatumika katika vyombo vya habari vya
serikali kila mara khasa wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu
unapokaribia lakini kwa kuwa serikali haitilii mkazo wasanii wake wa
ndani ya nchi wameshindwa angalau kumuandikia barua ya kumpa asante.
“Tume ya Uchaguzi na serikali yenyewe imeshindwa hata kuniandikia
barua angalau kunipa thanks ya kutunga na kutengeneza muziki huo ambao
unatumika kila mara unaohamasisha amani na utulivu nchini maana katika
mashairi yake yanasema sote ni ndugu na tuishi kwa amani” alisema.
Professa Ilyas alisema wakati wa awamu ya kwanza chini ya Rais
Nyerere na na Rais Karume fani ya muziki wa taarab ulithaminiwa sana
lakini hivi sasa vikundi vya muziki usiomuelekeo ‘modern taarab’ ndio
vinavyopewa kipaumbele zaidi kuliko muziki asilia.
Professa Ilyas alisema sio vyema kwa wasanii kuweka tamaa mbele na kuipotosha jamii kwa ajili ya kupata tonge kinywani.
Aliishauri serikali kuwatafuta wasanii wazuri na maarufu hapa
Zanzibar ili kuendeleza sanaa na maadili ya kizanzibari badala ya kuwapa
kipaumbele wasanii ambao wameweka kula zaidi kuliko kulinda maadili ya
nchi yao.
Mohammed Ilyas mbali na kubakia katika kikundi chake cha asili pia
anapiga taarab katika mahoteli maarufu nchini ikiwemo Serena Hotel na
mahoteli mengine ya kitalii yaliopo katika ukanda wa utalii katika
vijiji mbali mbali vya shamba.
Akimalizia Professa Ilyas alisema wasanii wanaweza kusaidia jamii kwa
hali nyingi huku akitoa mfano wa muimbaji maarufu nchini marekani
Michael Jackson alipoweza kuwahamasisha waimbaji wenzake kusaidia
wananchi wa Ethiopia wakati walipokumbwa na janga la njaa ambapo
walifanikiwa kutoa wimbo maarufu uliopewa jina la ‘We are the would
we are the children’ ili kukusanya fedha za kusaidia watoto wa nchi hiyo
waliokuwa wamekosa chakula huku nchi yao ukikubwa na njaa.
Hata hivyo alisema bado hajavunjika moyo na anategemea kuna siku nchi
yake itamkumbuka na itafahamu mchango wake aliotoa katika jamii ya
Zanzibar.
“Imani yangu kuna siku moja taifa langu litanitambua kama ni msaini bora hapa kwetu” alimalizia kusema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni