Nilianza kumfahamu Mzee yusuf katika ukumbi wa Equator Grill uliopo Mtoni kwa azizi ally, temeke, Dar es Salaam. Nilipenda sana jinsi alivyokuwa anapiga kinanda wakati huo, ” anasema mwimbaji nyota wa taarab wa kundi la Jahazi, Leila Rashid.
Anasema kipindi hicho alikuwa akihudhuria maonyesho mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na kikundi cha taarab cha Zanzibar Stars, ambacho mzee yusuf alikuwa mmoja wa wasanii wake, akiwa anapiga kinanda.
LEYLA RASHID AKIWAJIBIKA KATIKA MOJA YA VIDEO ZAKE. |
Leila, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji tangu akiwa mdogo anasema, alikuwa na kawaida ya kwenda kwenye ukumbi huo kila Zanzibar Stars ilipokuwa ikifanya onyesho.
“Nilikuwa na ndoto ya kuimba taarab tangu nilipokuwa mdogo na nilikuwa nikivutiwa sana na uimbaji wa Sabah Salum ‘Muchacho’ kutokana na uimbaji wake mzuri,” anasema.
Leila anasema alikuwa akitumia muda mwingi akiwa nyumbani kwao kuimba nyimbo mbalimbali za waimbaji nyota wa muziki huo kwa lengo la kupima uwezo wake kama anaiweza fani hiyo.
Mwimbaji huyo mwenye sura na umbo la kuvutia, ambaye wajihi wake unashabihiana na mwanamke wa kisomali, anasema siku ya kwanza kuanza kufahamiana na mzee yusuf, alijihisi mwenye furaha kubwa.
“Kwa kweli siku ya kwanza kufahamamiana na mzee yusuf nilijihisi mwenye furaha sana na niliamini ataweza kunisadia kukuza kipaji changu cha uimbaji nilichokuwa nacho,” anasema.
Baada ya kufahamiana na kuwa karibu na mzee yusuf, Leila anasema mwimbaji huyo gwiji wa taarab alimshawishi ajiunge na kikundi cha Zanzibar Stars, ambacho kilikuwa kikiwika wakati huo.
Leila, ambaye kwa sasa anasikika kila kona ya nchi kutokana na uimbaji wake mzuri, anasema ushauri aliopewa na mzee yusuf aliusikiliza na kuufanyia kazi.
Anasema alijiunga na Zanzibar Stars miaka 14 iliyopita na wimbo wake wa kwanza ndani ya kikundi hicho unajulikana kwa jina la ‘Riziki atoae Mola’.
Mwimbaji huyo mwenye bashasha anasema, baada ya kurekodi wimbo huo, hakufanikiwa kutoa wimbo mwingine kutokana na ubinafsi uliokuwepo katika kundi hilo.
LEYLA RASHID AKIIMBA SAMBAMBA NA MUMEWE MZEE YUSUPH. |
Anasema mara yake ya kwanza kupanda kwenye steji alikuwa na hofu, lakini alifanikiwa kuimba vizuri na kushangiliwa na mashabiki wengi.
Leila, mwimbaji mwenye sauti nyororo na macho ya kuvutia anasema, aliamua kuondoka Zanzibar Stars kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ubinafsi na uchache wa maslahi.
Anasema licha ya kwamba kipindi hicho Zanzibar Stars ilikuwa inatamba kwa nyimbo za taarab, maslahi yalikuwa madogo, hali iliyosababisha waimbaji wengi mahiri kuhama.
Mwimbaji huyo anasema, mwaka 2006 alijiunga na kundi jipya la Jahazi Morden Taarab ‘Wana wa nakshinakshi’ chini ya Mkurugenzi wake Mzee Yusuf.
Anasema kuanzishwa kwa kundi hilo, ambalo linaongozwa na mume wake, mzee yusuf kulimfanya afahamike ndani na nje ya nchi hii.
“Jahazi ndiyo imenifanya nifahamike kila kona ya nchi hii, nadhani kama si kundi hili, hadi sasa ningekuwa sifahamiki,” anasema.
Leila anasema wimbo wa ‘Maneno ya mkosaji’, ambao ulikuwa wa kwanza kuimba katika kundi hilo la jahazi, ulimpandisha chati na kumpa umaarufu mkubwa na kusisitiza kuwa, kwa sasa anajiona yupo kwenye chati ya juu.
WAIMBAJI WA JAHAZI MODERN TAARAB WAKIWA STEJI. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni