NA KAIS MUSSA KAIS.
+255657036328
“MAPENZI yangu pokea,kwa moyo wa ukunjufu
Wewe nnakulete,usiwe mbabaifu
Kama utayagomea,nitakujua dhaifu”.
Hio ni moja kati ya beti ya wimbo maarufu wa taarab asilia
unaojulikana kwa jina la ‘Mapenzi yangu pokea’ulioghaniwa na mutrib mashuhuri
na mkongwe ambae ameshastaafu,Maalim Mohammed Ahmed Mohammed.
Bila shaka jina hilo sio geni miongoni mwa wapenzi wa muziki
wa taarab asilia wa Zanzibar na hata nje ya visiwa hivi vya marashi ya karafuu.
MOHAMMED AHMED MOHAMMED AKIWA STEJINI. |
Licha ya kuwa Mohammed Ahmed ameimba miaka mingi
iliyopita,lakini nyimbo zake bado ni dhahabu masikioni mwa wengi kila
wanapozisikiliza zikipigwa katika vituo vya
redio au katika rekodi za cd.
Sifa za nguli huyu wa utunzi wa mashairi ya taarab na
uimbaji,zilimshawishi mwandishi wa makala haya kumtafuta ili kufanya mahojiano
naye,kwa dhamira ya kufahamu tarikh yake katika fani hiyo na siri ya mafanikio
yake.
Akisimulia Maalim Mohammed Ahmed alisema fani hiyo hakurithi
kutoka kwa mtu yoyote katika familia yake,bali yeye mwenyewe aliipenda pamoja
nay eye mwenyewe kuvutwa na ushawishi kutoka kwa wenzake.
Alieleza kuwa mnamo mwaka 1961,ndipo alipojitumbukiza rasmin
katika fani ya taarab kwa kujiunga na kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa chenye
maskani yake katika mtaa wa Kokoni Malindi.
Huko alikutana na wasanii wengi akiwemo marehemu Maalim Iddi
Abdallah Farahan,Marehem Maalim Seif Salim,Maalim Abdallah Suleiman na wengine
wengi.
Mara baada ya kujitosa kwenye klabu hiyo yenye historia ndefu
katika bahari ya muziki wa taarab Afrika Mashariki,msanii huyo amesema alianza
kwa kuimba wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Wanaodharau mapenzi yafaa tuwaapize’
wimbo ambao hapo awali uliimbwa na mwimbaji mwengine kundini humo.
Baadae alisema akaanza kuimba wimbo ‘Adam na Hawa’ uliotungwa
na Marehem Saleh Ajmi ambao alisema hata hivyo wimbo huo haukupata umaarufu
kwani uliimbwa mara moja.
Baada ya takriban miaka miwili nyimbo za kukopia na
zilizotungwa na watunzi wengine,Maalim Mohammed Ahmed alisema mwaka 1963
alianza kutunga na wimbo wake wa kwanza ulikuwa ni ‘Mapenzi yangu pokea’ ambao
mpaka sasa bado unapendwa.
Kuanzia hapo kasi yake ya utunzi ikapamba moto ambapo zipo
nyimbo alizotunga na kuimba mwenyewe na nyengine zikaimbwa na wasanii wengine
katika kundi lake hilo.
Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘Ua’
ulioimba na Almarhum Maalim Seif Salim ‘Kisebusebu’,Almarhum Bakari
Abeid ‘Kibiriti na Petroli’ Maalim Seif Salim,pamoja na ‘Sasa sinae’ulioghaniwa
na Almarhum Khamis Shehe.\
Mnamo mwaka 1964 wakati vikundi vyote vya Unguja vilipoungana
na kuunda kikundi kimoja cha Mila na Utamaduni,Mutrib huyu alikuwa miongoni mwa
wasanii waliojumuika kuanzisha kikundi hicho ingawa baadae aliondoka na kwenda
masomoni.
Lakini baada ya kurudi kutoka masomoni,alieleza kuwa uongozi
wa klabu ya Culture ulimuomba ajiunge nao na kumpa wadhifa wa Ukatibu,ingawa
halikumzuia kuendelea na Nadi Ikhwan Safaa.
Wakati nikizungumza na gwiji huyu alinambia ametunga nyimbo
nyingi sana,lakini nyengine amezisahau .
Hata hivyo,aliutaja mmoja wa wimbo alioutunga ambao aliupa
jina la ‘Kunguru’ ambapo alinambia aliutunga na kuuimba yeye mwenyewe.
Baadhi ya maneno yaliokuwemo katika wimbo huo ni kama
yafuatayo:
Kunguru ndege laghai,Anatabu kumnasa
Kama yeye hatokei,Mwenye hila na mikasa
Japo ukifanya rai,Weka mbele kumkosa.
Aidha Maalim Mohammed Ahmed alibainisha kuwa,hata klabu ya
Culture yenye maskani yake mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar,aliitungua nyimbo kadhaa
zikiwemo ‘Pesa’ ambao uliimbwa na msanii mkongwe Nihfadhi Abdullah, ‘Kukupenda
sana ‘Rukia Ramadhan’ Sikujua kama mapenzi
matamu nao ulighaniwa na bibie Mtumwa Mbarouk
Wimbo wa sikujua kama mapenzi matamu ulikuwa ukisema kama
hivi:
“Ni hakika sikujua kwamba, Mapenzi matamu
Si dhihaka nakwambia,Yatanitia wazimu
Hivi sasa natambua,Kwamba yamenilazimu
Kila nikiliridhia,Inazidi yangu hamu.
Mbali na wimbo huo pia alitunga wimbo Pendo letu
lishasibu ambao uliimbwa na mkongwe
mwengine na mwalimu katika jukwaa la sanaa za maigizo na tarab asilia Marehemu
Bakari Abeid Ali.
Muziki wa taarab umeweza kumfikisha mkongwe huyo katika nchi
mbali mbali duniani.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Kenya,Visiwa vya Comoro,Dubai na
Abudhabi,Oman,Hispania,Ubelgiji,Ufaransa,Uholanzi,Italia,Denmark,Uswisi,Finland,Visiwa
vya Reuniuon na nyenginezo.
Pia ametembela Mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara ambapo
alikwenda kutumbuiza na klabu zake kwa vipindi tofauti.
Nilipomuliza
anifafanulie tofauti anazoziona baina ya taarab asilia na ile inayoitwa ya
kisasa,Maalim huyo kitaaluma,kwa sasa hakuna watunzi wa maana bali waliopo ni
watu wanaotafuta maslahi pekee bila ya kuzingatia maadili na mambo muhimu
katika utunzi wa nyimbo za taarab.
Alifahamisha
kwamba wakati yeye anajiunga na taarab,ilikuwa lazima mtu alipie shilingi kumi
na baadae kila mwezi shilingi tatu kinyume na miaka hii ambapo msanii anajiunga
katika kikundi kwa matarajio ya kulipwa kabla hajaanza kutoa mchango wowote
kukiinua kikundi anachojiunga nacho.
“Kuna
tofauti kubwa kati yetu wasanii wa zamani na hawa wasanii wa sasa,sisi
tulikujwa hatulipwi bali tukilipia ada ya klabu,mimi mwenyewe wakati najiunga nililipa shilingi kumi na
kila mwezi wanachama sote tulikuwa tunalipa,leo wasanii wanalipwa wao” alisema.
Kuhusu
tofauti ya kimuziki,Maalim alisema hakuna kitu kinachoitwa modern taarab,bali
hiyo ni aina ya ngoma iliyoingia mjini na kwa kuwa kiingiacho mjini si
haramu basi mambo yanakwenda tu kama
yanavyoonekana.
“Taarab
lazima ipigwe kwa kutumia ala za asili kama vile qanoon,oud,fidla na
nyenginezo,lakini leo mtu unaweza kuwa na keyboard yako ukapiga taarab,mimi sijawahi kuona kama
wenzetu Tanga wanaita kumbwaya na Mombasa wanaita Chakacha basi na hapa kwetu Unguja watafute jina lakini sio
taarab,”alifafanua.
Nilitaka pia
kujua ni wasanii gani wanaomvutia katika kazi zao,naye bila ya kigugumizi
akawataja baadhi ya wasanii akiwemo Marehemu Rashid Sultan,Marehemu Bakari
Abeid,Marehemu Seif Salim,Ali Soud na Marehemu Maulid Mohammed Machaprala.
Hata
hivyo,kwa maneno yake,alieleza kuwa miongoni mwa wanawe hakuna anayeweza kusema
kwa uhakika kama anafuata nyayo zake za usanii,ingawa alimtaja mmoja wa watoto
wake aitwae Harusi kuwa anaonekana kujaribu kutaka kujiingiza katika tasnia
hiyo..
Nilipomtaka
atoe maoni juu ya dhana ya baadhi ya watu kuwa muziki ni uhuni,Maalim Mohammed
alikuwa na fikra nyengine tofauti na kusema kuwa uhuni ni tabia ya mtu kwani
wapo wahuni wanaojulikana sana katika jamii lakini kamwe hawafanyi kazi ya
muziki wala usanii wa aina yoyote.
“Hizi ni
dhana potofu muziki ni kazi kama kazi nyengine zinazoweza kumjengea mtu heshima
na kutambulika kitaifa na kimataifa,pia muziki umetumika katika kusaidia mambo
mbali mbali kwani una nguvu ya kuhamasisha.
Na zaidi
mbona mimi sijawa muhuni,Umkulthum,Abdelhalim Hafidh na wengine wengin
hawajakuwa wahuni,”alitoa mfano.
Juu ya siku
hizi kutokuwepo kwa watunzi wengi wa masihairi ya taarab,msanii huyo alisema
hiyo inasababishwa na muziki kugeuzwa biashara ,ambapo alisema watunzi wa sasa
wanataka kulipwa na walipaji hakuna .
Akitoa mfano
wa klabu za Malindi na Culture ambazo alisema zinashindwa kutoa nyimbo mpya
kutokana na kushindwa kulipia.
Mbali na
fani ya muziki,lakini msanii huyo aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali
Serikalini baada ya awali kuwa mwalimu mkuu katika skuli tofauti ikiwemo
Langoni, Wilaya ya Magharibi mwaka 1971,Ole(1972) Kisiwandui(1974) na baadae
mwalimu mkuu skuli ya Sekondari Shangani mjini Unguja.
Aidha
aliwahi kuwa Afisa wa Mambo ya Kale,Mkurugenzi Mipango Wizara ya mila na
Utamaduni,Katibu Muhtasi Ikulu Zanzibar,Katibu Muhtasi wa Rais Ali Hassan
Mwinyi Zanzibar,na Baadae Katibu Mkuu Afisi ya Rais.
Nafasi hiyo
ya Katibu Mkuu alianzia kipindi cha Rais Marehemu Idrissa Abdulwakil na
kuendelea mpaka wakati wa Rais Dr Salmin Amour Juma alipomaliza muda wake nae
akafikia muda wa kustaafu.
Kupitia
makala hii Maalim Mohammed Ahmed amewashauri wasanii wasikimbilie kuimba tu
bali wajifunze kwanza apamoja na kutafuta ujuzi wa kupia ala mbali mbali za
muziki wa taarab.
Alitoa mfano
wa kikundi cha taarab asilia kinachoundwa na wanawake watupu cha Tausi ambacho
kinawafundisha wasanii wake kuimba pamoja na upigaji wa ala.
Pia aliwaasa
wasanii kuacha tabia ya kupikiana majungu na fitina katika vikundi ili kuepusha
kuvunjika kwa vikundi hivyo.
Msanii huyo
aliyebaki kuwa miongoni mwa mifano ya kuigwa alizaliwa mwaka 1940 katika mtaa
wa Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja akiwa motto wa kwanza katika familia
ya watoto watano wawili wakiume na watatu wakike.
Alianza
kupata elimu ya msingi mwaka 1946 katika skuli ya ambayo wakati huo ikiitwa
Mnazi Mmoja kuanzia darasa la kwanza hadi la pili ambapo skuli hiyo hivi sasa
imekuwa kituo cha American Corner.
Baadae
alihamia skuli ya Gulioni huko alisoma mpaka darasa la sita na kuhamia
Kiembesamaki kwa masomo ya darasa la saba na la nane kabla ya kujiunga na
‘Junior Secondary School’ ambayo kwa sasa ni Benbella kuanzia kidato cha kwanza
hadi cha tatu.
Mnamo mwaka
1961 alijiunga na Chuo cha Ualimu na kuanza kusomesha mwaka 1962.
Ilipofika
mwaka 1976 alijiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa
ngazi ya ‘Bachelor of Education’ na kumaliza mwaka 1979.
Mwaka 1983
alikwenda nchini Uholanzi kuendelea na masomo yay a digrii ya juu (Masters).
Gwiji huyo
ameoa na amejaaliwa kupata watoto na pamoja na kustaafu taarab,amesema hupata
wasaa wa kujikumbusha kuimba hususan katika shughuli maaalum ikiwemo harusi za
familia yake... Makala hii kwa hisani ya Bin Mahmoud.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni