NA KAIS MUSSA KAIS.
“NIKUMBATIE mwenye wivu atazame,Nikumbatie roho yake imuume
Nikumbatie mwenye wivu
alalame,Nikumbatie akujue wangu mume
Njiani nikipita arudi kinyume nyume,Kata kiu yeye Fanta mi
sina habari nae
Ajijue cheo chake mina yeye hatufanani,Atuone ashituke anijue
mimi nani
Cheza na mimi mpenzi cheza name kwa helenzi,Mambo mazuri
laazizi ndo hayataki haraka”
|
BI RUKIA RAMADHAN. |
Ni moja ya beti katika nyimbo maarufu za muziki wa taarab
visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wa wimbo unaojulikana kwa jina la
‘Nikumbatie’ ambao uliimwa katika kundi maarufu la East African Melody.
Maneno hayo ni miongoni mwa wimbo mzima ulioghaniwa na
mwanadada mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni sie mwengine bali ni bibie Rukia
Ramadhani Ali.
Rukia ni msanii mahiri katika anga la muziki wa taarab ndani
nan je ya Tanzania ambae kila kona ya dunia anajulikana kutokana na kipaji
chake alichojaaliwa na muumba wake.
Msanii huyo ambae hapendelei kuitwa malkia wa mipasho kutokana na kutopendelea kuimbwa nyimbo za
kupashana na kuelekeza zaidi nguvu zake katika nyimb o za mahaba na
kubembeleza.
Nilipomuuliza anajiskiaje kuitwa jina hilo la malkia wa
mipasho,hakuonesha bashasha wala haiba yake ya kawaida ya kutabasamu na akajibu
‘sitaki kuitwa malkia wa mipasho kwa sababu siimbi wala sifikirii kuimba
mipasho’.
Jibu hilo lilinifanya nishangae kidogo kwa vile nyimbo za
mipasho ndio zaidi hivi sasa zinazowapa umaarufu mkubwa waimbaji wake kiasi cha kumuuliza nini sababu
ya msimamo wake huo.
“Mimi ni msanii ninaependa zaidi taarab asilia ambayo lugha
ya mashairi yake ni ya kiungwana,haina maneno makali tofauti na taarab ya
kisasa,wanaimba tu lakini haina maadili ya Kizanzibari au taarab kwa
ujumla,”alisema bila ya kutaka kuingia ndani zaidi.
Nilipotaka kujua alipoanzia hadi alipofikia,Rukia hakukataa
tulikwenda hatua kwa hatua hadi mwisho wa mazungumzo yetu,alipoanzia alipofikia
na matarajio yake ya baadae.
Msanii huyo alisema alijitosa rasmin katika fani ya muziki
mwaka 1974 katikam kikundi cha Tawi la Afro Shirazi Party la Mwembeshauri chini
ya mwalimu wake Marehemu Khamis Shehe.
Alisema wakati huo walikusanywa watoto wengi wa mtaani hapo
kwa ajili ya kufundishwa masuala ya uimbaji na baada ya mafunzo ya muda walipelekwa
majaji wenye uelewa mpana wa muziki huo na uimbaji kwa kuwachuja vijana hao.
Rukia alikuwa miongoni mwa vijanan waliopenya katika mchujo
wa majaji hao na hapo ukawa mwanzo wa mafanikio
yake kwa vile kupita huko kulimfanya apelekwe katika klabu maarufu ya
tab visiwani humu ya Culture Musical Club yenye maskani yake katika mtaa wa
Vuga mjini Unguja.
Alianza mazoezi katika klabu hiyo na hatimae kuanza kuimba
akiwa bado mwanafunzi wa shule na hivyo kuweza kubeba majukumu yake yote ya
usanii na masomo shuleni.
Alisema alianza rasmin kuanza kupanda jukwaani akiwa na kundi
lake la Culture na nyimbo yake ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Kukupenda
sana ndilo kosa langu sitofanya tena naapa kwa Mungu,Nilioyaona yanatosha
kwangu’.
Kutoka kwake huko kuliwashtua wazazi wake ambao waliona
kwamba anajikita zaidi katika maswala ya nuimbaji,badala ya kuzingatia masomo
yake hivyo ilimsababishia kuhamishwa
Zanzibar na kupelekwa Dar es Salaama
kuendelea na masomo.
Msanii huyo mahiri alieleza kwamba alikaa jijini humo kwa muda wa miaka minne
na kuendelea na masomo katika shule ya msingi ya Temeke kabla ya kurejea Unguja
kuendelea na masomo yake katika shule ya Rahaleo,Kidutani ndogo na kubwa ambapo
alimalizia kidato cha nne.
Kurejea kwake Unguja kulimfanya arudie tena kwenye muziki wa
taarab na kwa bahati mbaya au nzuri hakurejea tena katika kundi lake la awali
bali alihamia kwenye kundi mama la Nadi Ikhwan Safaa.
Alisema akiwa ndani ya kundi hilo,lenye maskani yake katika
mtaa wa Kokoni mjini Unguja alikweza kuimba nyimbo kadhaa ambazo ziliweza
kumjengea jina na kumpa umaarufu zaidi.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Nnazama, Nadra na
Sadfa,Hidaya, Baada ya dhiki faraja,Niapishe na nyiengine nyingi ambazo zote
hizo zinaendelea kupendwa hadi hivi sasa.
Rukia alisema kuanzishwa kwa kundi jipya la taarab la Bwawani
ambalo lilikuwa linamilikiwa na hoteli ya Bwawani kulimfanya ahame katika kundi
lake hilo na kuhamia katika kundi la Malindi chini ya msanii mahiri Marehemu
Mwalimu Abdallah .
Alisema kikundi hicho cha Bwawani hakikudumu muda mrefu sana
kwa vile kilivunjika,lakini kabla ya kuvunjika msanii huyo alifanikiwa
kukiimbia kikundi hicho nyimbo kadhaa zikiwemo Nidhibiti,na Nadekea change.
Baadhi ya maneno yaliokuwemo katika nyimbo ya Nidhibiti ni
kama hivi
Nidhibiti unitunze,Nitunze nihifadhike
Nihifadhi wanyamaze,Nipoe nitononoke
Raha zako nieneze,Milele milele nifarijike
Miti shamba wamalize,Halafu waweweseke.
Rukia ambae ni miongoni mwa wasanii waanzilishi wa kundi la
‘The East African Melody’ ambalo llilianzishwa nchini Dubae mwaka 1992,akiwa na
wasanii kadhaa.
Akiwa nchini humo nyimbo za mwanzo alizoimba ni pamoja na
Karibu habibi,Nimesharidhika na Nasubiri miujiza na baadae kundi hilo lilihama
nchini Dubae na kuhamia visiwani Zanzibar.
Katikati ya mwaka 2000 msanii huyo alipumzika kuimba kwa muda
wa mwaka mmoja hadi mwaka 2001 aliporejea tena kwenye ulingo wa taarab na kundi
lake hilo la East African Melody.
Mara baada ya kurejea tena msanii huyo alionekana kuendelea
kuvutia zaidi kutokana na kuimba nyimbo
zake kadhaa ambazo zilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi wa muziki wa
taarab .
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Njoo Habibi,Nani kama
wewe,Wastara hasumbuki,Kufa na tai shingoni,Nataka ridhaa yako,pamoja na nyimbo
ya Nikumbatie.
Mbali na kuimba Rukia anamudu saana sanaa ya uigizaji ambapo
aliwahi kuigiza mchezo wa ‘Mkombozi wa Mwafrika’ambapo alisema kwamba uimbaji
uliweza kumletea matatizo kutoka kwa watu mbali mbali ikiwemo kumtishia kumpiga
na hata wengine kutaka kumuwekea sumu kwenye chakula.
Pamoja na kutishiwa huko na vitisho hivyo msanii huyo
alikabiliana na changamoto hizo ambazo hazikumkatisha tama na kuendelea na
shughuli yake hiyo aliyokiri kuipenda ndani ya damu yake.
Rukia hakufafanua kwa nini alitishiwa,lakini alisema hayo ni
mambo ya zamani na kwa sasa ayameshapita.
“Kwa kweli nilipokuwa najiunga na mambo ya sanaa nilipata
tabu saana kwani nilitishiwa kupigwa na hata kuambiwa nitatiliwa sumu kwenye
chakula lakini hayo yalikua mambo ya zamani sasa hivi hayapo,”alisisitiza.
Kuhusu maswala ya faida katika fani ya sanaa,Rukia alisema
muziki wa taarab umeweza kumsaidia kupata faida nyingi ikiwemo
umaarufu,kuheshimiwa na watu wa rika mbali mbali pamoja na kusafiri.
Alizitaja nchi alizotembelea kupitia muziki wa taarab ni
pamoja na Mikoa mbali mbali ya Tanza
nia,Kenya,Msumbiji,Comoro,Nigeria,Misri,Dubae,Oman,Abu Dhabi,Jamhuri ya
Dominica,Ufaransa,Uswiss,Ubelgiji,Italia,Uholanzi,Slovenia,Ujerumani,Japan,Marekani
na Uingereza.
Rukia alisema mpaka sasa kwa yeye ni taarab asilia ambayo ndio
mwalimu wake katika fani hiyo lakini pia hiyo haimzuii kuimba taarab ya kisasa.
“Taarab asilia ndio taarab hizi nyengine tunaimba tu kufuata
wakati,mimi siwezi kuidharau kwa kuwa ndiko nilipoanzia,”alifahamisha.
Akizungumzia juu ya tabia ya wasanii kuhama hama vikundi mara
kwa mara ,alisematabia hiyo sio nzuri ,lakini ijulikane kwamba msanii hawezi
kuhama bila ya sababu maalum.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuhama kwake hakutokani
na maslahi,bali kutokana na matatizo mbali mbali yaliokuwa yakijitokeza.
Msanii huyo hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa
wasanii mbali mbali ambao walimuwezesha kudumu katika fani hiyo akiwemo
marehemu Asha Simai,marehemu Khamis Shehe na Mohammed ilyas.
Kwa vile hakuna msanii
yoyote ambae hana msanii anaemvutia ,kwa upande wake Rukia alisema anavutiwa na
uimbaji wa wasanii wengi akiwemo marehemu Asha Simai,Marehemu Abdulaziz Yussuf
na Profesa mohammed Ilyas.
“Marehemu Bi Asha Simai alikuwa akinivutia mno katika fani
yake ya uimbaji hasa nyimbo ya iwapi ile ahadi, inanisuuza roho yangu Namuomba
Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake,”alisema msanii huyo.
Hivi sasa Rukia Ramadhani ni muimbaji huru ambae anaimbia
vikundi tofauti anapopata mualiko kikiwemo kikundi cha Zanzibar One Modern
Taarab na vikundi vyengine.
Pia msanii huyo ni mwalimu wa sauti(kuimba) katika Chuo cha
Muziki wa nchi za Jahazi(DCMA) ambapo aliwataka wasanii kujifunza zaidi mara wanapoingia katika fani hiyo.
“Nawashauri wasanii kujifunza zaidi kusoma muziki ili waweze
kujifahamu na kuelewa nini wanachokifanya jukwaani kwani wasanii wengi hawataki
kujifunza.
Rukia Ramadhani Ali ni mtoto pekee wa bwana Ramadhani Ali na
Bi Zuhura ambapo mbali na fani ya usanii lakini pia ni muajiriwa wa serikali
katika Wizara ya Katiba na Sheria...Makala hii kwa hisani ya Bin Mahmoud.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni