TANGAZA NASI

Breaking

Ijumaa, 18 Mei 2018

KHADIJA MBEGU CHIPUKIZI ANAE TINGISHA KWA SASA, JE UNAJUA ALIANZIA WAPI?.

Na pambe za taarab.

    Muziki wa taarab unazidi kushika kasi kwa sasa hususani baada ya kuendelea kuzaliwa bendi kadhaa ambazo nimekuja kuzidisha ushindani ambao ulionekana kupotea kipindi cha kati nazo ni first class inayoongozwa na Prince amigo, five stone iliyo chini ya Juma mkima, halichachi classic ambayo inaongozwa na Amour magulu na nyingi nyinginezo.

Jina la khadija mbegu au ukipenda unaweza kumuita "khadija kais" ni ingizo jipya kabisa katika tasnia hii, msichana huyu mwembamba mrefu kiasi na asiye na majivuno naweza kusema ni miongoni mwa wale waliojaaliwa vipaji vya kuimba na mwenyezimungu na anajua kutumia kipaji chake haswa akiwa stejini, mtandao huu ulimtafuta ili kupata mawili matatu tokea kwake na kwa bahati tulimkuta nyumbani kwao kwa wazazi wake mbagala jijini dar es salaam maeneo ya "kwa dumbalume" na mahojiano yalikuwa yalikuwa kama ifuatavyo:-

Pambe za taarab:- Habari yako khadija, sisi ni wandishi tokea mtandao bora wa taarab nchini tanzania, tunapenda kujua historia yako kimuziki maana wasomaji wetu wamekuwa wakihitaji sana kujua ni wapi umetokea maana wanaona umeibuka tu na kuanza kufahamika, ni wapi ulipoanzia mpaka kufikia hapo?.

Khadija mbegu:- Kwanza nianze kwa kuwashukuru kwa kunitafuta mpaka mmeweza kufika huku kwetu mbali kiasi hiki, mungu awabariki sana, mimi kiukweli sina muda mrefu katika muziki huu wa taarab, nilikuwa naupenda muziki huu toka zamani lakini sikuwaza kuwa ipo siku nitakuwa muimbaji kama hivi, ilikuwa siku moja nimeenda kusuka huku huku kwetu mbagala nikakutana na Salha abdallah yule aliekuwa mke wa hammer Q, sasa kuna wimbo ulikuwa ukiimbwa ktk redio nami nikawa naufuatisha aliponisikia akasema wewe msichana mbona unajua kuimba sana!, kwani unaimbia bendi gani? nikamjibu mimi nipo tu nyumbani wala siimbi popote, ndipo akaniambia kesho twende mazoezini kwetu wakaliwao modern taradance kwa thabit abdul akusikilize unaonekana una kipaji sana basi nami nikamjibu sawa haina shida.

Pambe za taarab:- Ekhe vipi sasa ulifanikiwa kwenda huko wakaliwao au uliingia mitini kwa hofu? funguka mama!.

Khadija mbegu:- Mwenzangu we acha tu!, nilienda ndugu yangu nilipofika thabit abdul akanipigia vyombo kwa mara ya kwanza nikaimba wimbo uitwao "fungu la kukosa" wa bendi hiyo hiyo wakaliwao. Aliponisikia akasema uwezo wangu bado ila niwe naenda mazoezini kila siku nitakuwa vizuri maana kipaji ninacho. Basi nikawa naenda mazoezini na siku zingine naenda mpaka katika show zao! Ila kuna siku sitoisahau tulikuwa tunafanya show pale magomeni maeneo ya mwembechai karibu na shekhe Yahya hussein, thabit alisema kuanzia siku hiyo nisipandishwe stejini wala nisiruhusiwe kuimba sababu sijui. Basi nikarudi nyumbani nikawa siendi tena nafanya issue zangu zingine tu hapa home.

Pambe za taarab:- Sasa ilikuwaje tena mpaka ukaibuka na kuanza kuwa maarufu wakati uliamua kukaa nyumbani khadija?.

Khadija mbegu:- Nakumbuka siku moja nilikutana na kaka kais mussa kais akaniuliza unaimbia bendi gani kwa sasa? nikamjibu kuwa nipo tu nyumbani sina bendi, akachukuwa simu yake hapo hapo akampigia mkurugenzi wa jahazi kolombwe Chollo akamwambia huyu khadija ni ndugu yangu mpokee na umpe kazi, basi hapo ndio ukawa mwanzo wa safari yangu ya mafanikio kiuimbaji. Nilikaa jahazi kolombwe kama miezi nane tu! nikawa vizuri haswa ndipo kaka kais mussa kais tena kwa mara ingine akanipeleka jahazi modern taarab yenyewe sasa baada ya wasanii wengine kuhama na mzee yusuph kuacha bendi.

Pambe za taarab:- Wakati unaenda jahazi modern taarab uliwakuta wasanii gani wakongwe? na vipi hukuhofia kwakuwa umeingia ktk bendi kubwa kuliko uliyotoka?.

Khadija mbegu:- Pale niliwakuta fatma Kasim, mwasiti kitoronto, Mishi zele, zubeda mlamali, Mossi suleiman na wengineo nakumbuka chipukizi nilikuwa peke yangu tu, nilipewa jukumu la kuimba nyimbo zote za fatma mcharuko ambae alikuwa amehamia yah tmk modern taarab, kiukweli nilizitendea haki nyimbo zile maana nilikuwa nikiziimba kama yeye mwenyewe haswaa! jambo ambalo liliniongezea umaarufu zaidi na jina langu kukuwa zaidi na zaidi. Nilianza kutafutwa na wandishi kwa mahojiano na interview mbalimbali za redio nilifanya za nchini na nje ya nchi.

Pambe za taarab:- Sawa sawa!, hapa kati tumepenyezewa ubuyu kwamba umeondoka jahazi modern taarab na unaonekana gusagusa min bendi huku pia ukionekana mazoezini kwa bendi mpya ya amigo first class modern taarab hapa ikoje?.

Khadija mbegu:- Ahsante sana kwa swali zuri sana ambalo nami pia napenda wapenzi na wadau wangu wajue, mimi ni msanii na bado nipo ktk kujifunza kama ambavyo nilikutana na Sada nassor akanipa ushauri. Nyimbo za zamani kama zilizoimbwa na akina fatma issa, malika, bi rukia na wengineo zina njia haswa za uimbaji na muimbaji bora wa taarab ni lazima aweze kuimba nyimbo zile, nami nilikuwa sizijui nikapelekwa gusagusa min bendi na kaka kais mussa kais ili nijifunze zaidi na nashukuru kwa sasa naziimba vizuri sana mpaka nimeshaanza kuwa na wapenzi pale gusagusa!, sasa pale first class nilizungumza na mkurugenzi wangu Hassan farouk akaniruhusu wala haina shida maana first class wanaimba taarab ya kisasa na gusagusa tunaimba old is gold ni vitu viwili tofauti kabisa!. Unajua watu siku zote wanapenda kuona mtu unaharibikiwa nasikia tayari wameanza kupandanisha maneno kwa viongozi wangu bila kujua nini kinaendelea na watu hao nawajua kwa majina sema sina muda wa kuwajibu nawaacha waendelee kuporojoka!.

Huyo ndie khadija mbegu au ukipenda muite khadija kais chipukizi mwenye ndoto ya kufika mbali kimafanikio ndani ya muziki huu wa taarab nchini tanzania, mtandao wa pambe za taarab tunamtakia mafanikio katika safari yake hiyo ya muziki na tunampa ushauri anatakiwa awe mvumilivu kwani sehemu yoyote yenye mafanikio mitihani ni kitu cha lazima inampasa apambane na amuombe mungu zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni