TANGAZA NASI

Breaking

Jumamosi, 6 Desemba 2014

IJUE HISTORIA YA MAREHEMU BI KIDUDE KATIKA MUZIKI WA TAARABU NCHINI!.

NA KAIS MUSSA KAIS

Kama binadamu anaweza kufikia kupewa heshima ya kuwa “taasisi”(institution) katika jambo fulani basi marehemu Bi.Kidude aliweza kuwa mmojawapo. Ukiiweka mezani historia ya muziki wa taarabu na tamaduni za unyago visiwani Zanzibar ni wazi kwamba katika meza hiyo pembeni yake ni lazima aketi marehemu Bi.Kidude. Uzoefu na uelewa alionao katika idara hiyo ulikuwa hauna mpinzani. Inaaminika kwamba ndiye alikuwa mwanamke,mwimbaji mkongwe kupita wote Afrika Mashariki na Kati kabla ya kifo chake.
Picha hii ni kwa hisani ya Marcel Mutsaers aliyompiga marehemu Bi.Kidude wakati wa Tamasha lijulikanalo kama Festival Mundial kule Tilburg-Uholanzi mwezi June mwaka 2006.
Umri wake halisi haukujulikana. Kilichokuwa kinajulikana ni kwamba alikuwa na umri zaidi ya miaka 90 na mpaka anakufa sio ajabu alikuwa ameshafikisha umri wa miaka 100! Alikuwa muimbaji tangu miaka ya 1920 akiwa ni mfuasi wa Sitti Bin Saad mmojawapo wa waimbaji wa mwanzo kabisa wa taarabu visiwani Zanzibar.
Alikuwa anatambulika na kuheshimika kama malikia wa taarabu na mambo ya unyago asiye na mpinzani. Alizaliwa katika kijiji cha Mfagimaringo katika familia ya watoto saba. Jina alilopewa na wazazi wake alipozaliwa ni Fatuma Binti Baraka kabla jina maarufu la Bi.Kidude halijashika baadaye alipoanza kuwa maarufu katika uimbaji.Wazazi wake walikuwa ni wafanyabiashara ya kuuza nazi enzi hizo za Zanzibar iliyokuwa chini ya utawala wa wakoloni.
Katika mahojiano mbalimbali aliyofanya na vyombo tofauti tofauti vya habari ulimwenguni kipindi cha uhai wake marehemu Bi.Kidude aliwahi kusema alianza kuimba akiwa na umri mdogo wa miaka 10. uimbaji alijifunza kutoka kwa Sitti binti Saad tena kwa kujificha nje ya nyumba na kumsikiliza Sitti binti Saad akiwaimbia wageni ambao mara nyingi walikuwa wakipelekwa pale na yeye marehemu Bi.Kidude.
Akiwa na umri wa miaka 13 tu hakuwa na jinsi bali kukimbilia Tanzania bara(Tanganyika enzi hizo) ili kuepuka kuozeshwa kwa nguvu. Akiwa Tanzania bara alizunguka kila kona ya nchi akiwa muimbaji katika makundi mbalimbali ya muziki wa taarabu likiwemo lile maarufu la Egyptian Musical Taarab. Baadaye alihamia nchini Misri kwa kifupi kabla hajarejea kisiwani Zanzibar mahali ambapo aliishi mpaka umauti ulipomfika.
Mbali na uimbaji marehemu Bi.Kidude pia alikuwa ni mfanyabiashara.Anauza “wanja” na “hina” ambazo alizitengeneza mwenyewe. Pia alikuwa mtaalamu wa dawa za mitishamba lakini zaidi ya yote alikuwa Mwalimu wa “unyago” ambapo alikuwa na chuo chake mwenyewe huku akijivunia rekodi kwamba katika wanafunzi wake wote hakuna ambaye ameshawahi kupewa talaka na mumewe. Pengine hii ndio sababu mwaka 2004 ulipozuka umbea kwamba marehemu Bi.Kidude amefariki dunia wakati alipokuwa katika ziara ndefu ya kimuziki Ulaya na Mashariki ya mbali, kila mtu kisiwani Zanzibar alishikwa na butwaa na majonzi! Kwa bahati nzuri habari za “kifo” chake zilikuwa ni uzushi tu.


Mwaka 2005 huko Gateshead, Newcastle nchini Uingereza,marehemu Bi.Kidude alipokea tuzo yenye heshima kutoka World Music Expo (WOMEX) kwa mchango wake katika muziki na utamaduni wa Zanzibar. Katika kinyang’anyiro hicho aliwashinda wanamuziki mahiri kama Peter Gabriel, Miriam Makeba na wengineo. marehemu  Bi.Kidude aliwahi kusema kwamba hawezi kuacha kuimba mpaka siku atakapoiaga dunia kwani akiimba anajihisi kuwa binti wa miaka 14!
Mwaka 2006, kampuni ya nchini Uingereza iitwayo ScreenStation kwa kushirikiana na Busara Promotions walitoa documentary iitwayo “As Old As My Tongue-The Myth and Life of Bi.Kidude” iliyokuwa ikielezea historia nzima ya maisha yake Bibi yetu huyo. Alikuwa anakunywa pombe na pia anavuta sigara ,lakini zaidi ya yote alikuwa ni mahiri wa kuimba bila hata kutumia spika ya mdomo yaani microphone. mwenyezimungu akupe kauli thabiti, na kaburi lako liwe ni nuru miongoni mwa nuru za peponi AMIN!.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni