TANGAZA NASI

Breaking

Jumatatu, 18 Mei 2015

AMANI MBILO:- NAWAPENDA SANA DIDA NA MISH B!, NAVUTIWA NA UTANGAZAJI WAO MZURI!.


NA KAIS MUSSA KAIS.
        0657- 036328.

               Habari za jumatatu tulivu wapenzi wasomaji wangu, leo tumekutana tena hapa hapa katika kipengele chetu cha mjue mtangazaji wako, na bado nazunguka nje ya mipaka ya mkoa wa Dar, nimepata bahati ya kufanya mahojiano na mtangazaji wa redio Bomba Fm mbeya 104.0 Anaitwa Amani Mbilo au ukipenda muite mjukuu wampiga miti, yeye anatangaza kipindi cha taarab kiitwacho "Jipe raha".
AMANI MBILO a.k.a. AMMY AKIWA KAZINI.


      Kwanza nilipenda kujua jina lake kamili sambamba na elimu yake hasa aliipata wapi na sehemu gani ambazo amepitia katika ufanyaji wake kazi tokea amalize kusoma, nae alianza kwa kusema.


AMANI MBILO:-  Jina langu kamili ni Amani Mbilo a.k.a. Ammy "mjukuu wa mpiga miti" mngoni wa kwanza kutangaza taarab, watu wamekuwa wakishangazwa sana na jina la mpiga miti, leo napenda niwape ufafanuzi, ni kwamba hili ni jina halisi kabisa la babu yangu mzaa baba kwahiyo wasiwe na mashaka kuhusu jina hili. Elimu yangu ni ya chuo diploma nimesoma Dar es salaam school of journalism "DSJ" na nilianza kupata uzoefu hapo redio maria Dar ndipo nikaja hapa mbeya ambapo nilianza kufanya kazi kituo cha Generation Fm mbeya, baadae niliacha na kupata kazi ingine studio ya kutayarisha vipindi vya redio na matangazo nikiwa kama mtayarishaji [producer] baadae nilijiunga na Bomba fm redio mbeya ambapo nipo mpaka sasa nafanya kazi. Matarajio yangu ya baadae ni kuja kufanya kazi shirika la habari la BBC na namshukuru mungu nimeanza kufanya nao kazi katika "BBC MEDIA ACTION".


UBUYU WA TAARAB:-  Ni kwanini uliamua kutangaza vipindi vya taarab na sio vipindi vingine vya jamii na vipi unakumbuka ulivyoanza kutangaza taarab siku ya kwanza ilikuwaje?.


AMANI MBILO AKIWA KWENYE POZI.

AMANI MBILO:- Mimi kwanza kabisa sikuwa na hobi ya kutangaza vipindi vya taarab nilikuwa napenda kutangaza vipindi vya burudani lakini sio taarab, sasa ilitokea mtu wa kufanya kipindi cha taarab alikwenda kufunga ndoa na mchumba ake, nikachaguliwa mimi nishike kile kipindi kwa muda ndipo nilipoonekana nakipatia basi nikakabidhiwa moja kwa moja mpaka leo.


UBUYU WA TAARAB:- Ukiwa mdau na mtangazaji wa vipindi vya taarab nchini unaizungumziaje kilimanjaro music award's mwaka huu hususani katika vipengele vya taarab?.


AMANI MBILO:- Kiukweli kwa mtazamo wangu kili music award's walikuwa na wakati mgumu sana katika kupendekeza wasanii na bendi kwasababu sasa kuna bendi nyingi na zote zinafanya vizuri mimi nilikuwa nadhani wangejaribu kuangalia bendi zingine na wasanii wengine wachanga ili kuwapa moyo na kuukuza muziki huu, sasa kila mwaka wakiwa wanamtazama Mzee yusuph, Isha mashauzi, Khadija kopa na wengineo wenye majina makubwa, muziki huu utakuwa hauna jipya!.


UBUYU WA TAARAB:- Kwa mtazamo wako unadhani muziki huu kwa sasa unaporomoka katika soko la ushindani au unazidi kukuwa?


AMANI MBILO:- Muziki huu kwa sasa umekuwa ukipanda haswa kwa huku mikoani, mkoa kama wa mbeya ni moja ya mikoa migumu kukubalika muziki wa taarab, lakini naweza kukuambia kwa sasa mbeya umekuwa ni mmoja wa mikoa inayopenda taarab sana zaidi ya sana!.


UBUYU WA TAARAB:- Ni watangazaji gani wa taarab hapa nchini ambao kwa namna moja ama ingine unawapenda na kuwakubali kwa kazi zao?.

AMANI MBILO MTANGAZAJI WA BOMBA FM MBEYA.

AMANI MBILO:- Mimi nawapenda sana Khadija shaibu "Dida" wa times fm Dar na Mwanahamisi Bashiry mwenda au "Mish B" wa magic fm Dar.hawa naweza kusema ni kioo kwangu kwani nimekuwa nikiwafuatilia sana utendaji wao wa kazi na wananivutia sana!.


UBUYU WA TAARAB:- Mwisho una ushauri gani kwa watangazaji wenzio maana mmekuwa mkishutumiwa kwamba mmekuwa na tabia za upendeleo wa kucheza nyimbo za mabendi maarufu tu yaani mnabagua na kuziacha hizi bendi changa zisizojulikana.


AMANI MBILO:- Ushauri kwa watangazaji wenzangu ni kwamba siku zote msikilizaji anaongozwa na sisi watangazaji, na sisi watangazaji tuna uwezo mkubwa wa kumshawishi msikilizaji, tuwape nafasi ya kuweza kuchagua nyimbo wazitakazo kuzisikiliza, na kweli tuwachezee na sio kuendelea na mpangilio wetu ambao mtangazaji unapoingia studio unakuwa umeupanga. wasikilizaji ni watu muhimu sana kwetu.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni