TANGAZA NASI

Breaking

Jumatatu, 11 Mei 2015

DAWA YA WALE WOTE WENYE ACCOUNT FEKI NA WANAOTUKANA MITANDAONI YAPATIKANA!.






NA KAIS MUSSA KAIS.

               Asalaam aleykum wasomaji wangu, leo tumekutana tena katika uwanja wetu wa makala ya wiki kama ilivyo ada yetu ili kukumbushana mambo kadhaa wa kadhaa na kuelimishana zaidi.


      Leo nitazungumzia Wadau wa taarab na harakati zao katika kuufikisha mbali na kuushusha chini kabisa muziki huu wa taarab nchini, kuna baadhi ya wadau wa muziki huu wamekuwa wakiufanya muziki huu kuonekana wa kihuni na usio na adabu kutokana na matusi yao ambayo wamekuwa wakitukana haswa kupitia mitandaoni bila kujali kuwa wazazi wetu pamoja na viongozi wa nchi wamekuwa wakisoma matusi yao humu!.


     Ilikuwa ni Jumatatu ya wiki iliyopita nilipokea simu kwa namba nisiyoifahamu, huyo mtu akanisalimu na kuniuliza wewe ndie Kais Mussa Kais ambae unamiliki blog ya ubuyuwataarabutz.blogspot.com? nikamjibu kuwa ndie haswa! akaniambia siku ya jumatano niende "Basata" makao makuu nimuulize mtu fulani nisingependa kumtaja jina kutokana na nafasi yake aliyonayo serikalini nae mwenyewe hakupenda kutajwa mtandaoni. Basi siku ya jumatano nilifunga safari mida ya saa nne asubuhi kuelekea Basata, nilipofika nilimuulizia mwenyeji wangu nikaelekezwa zilipo ofisi zake!. Nilipofika nikajibiwa na katibu wake kwamba ana mgeni na nisubiri kidogo.


   Baadae niliingia na kujitambulisha kwake, Alinipokea vizuri na kuanza mazungumzo yetu rasmi. Kwanza alianza kunipongeza kwa harakati zangu ninazo zifanya na kunipa moyo kuwa atahakikisha ananipigania popote pale ili kuhakikisha nafika mbali na lengo langu linatimia, Pili alikuja kwenye pointi ya mazungumzo yetu, alianza kwa kusema kwamba Wadau wa taarab wamekuwa wakitukana sana matusi mazito tena ya nguoni mitandaoni alafu kwa taarifa tu ni kwamba viongozi wakubwa wizarani kwetu wanaona na lawama zimekuwa zikija hapa BASATA na TCRA, mbona watu wa Dansi wana magroup humo humo mitandaoni na hawatukanani?.


      Kwa sasa taarab inaonekana kama ni muziki wa kihuni usio na heshima kwa ajili ya hawa mashabiki ambao wamekuwa wakitukana kila kukicha humo mitandaoni tena kupitia kwenye magroup yenu! ninyi kama "ma-admin" mnatakiwa muwe wakali msiruhusu hali hiyo kuendelea kwani itakuja kuwaletea madhara hapo baadae.


     Labda nikueleze tu kwamba wiki mbili zilizopita Wizara na viongozi wa TCRA tulikuwa na kikao kujadili wachafuzi wa hali ya hewa mitandaoni na mifano mingi imekuwa ikitolewa kwenu watu wa taarab na haswa ninyi ma-admin je mnapoona matusi toka kwa wanachama wenu mnachukua hatua gani?,  Basata kupitia wizarani tukishirikiana na TCRA tumeandaa mpango endelevu katika kuwadhibiti hawa wanaotukana matusi na kutoa maneno ya kashfa mitandaoni hata kama watatumia account feki mtambo tutakaoufunga utakuwa unamonita eneo alilopo mtuma posti na ametumia simu au kompyuta kila kitu chake kitakuwa kimejulikana wazi wazi bila kificho.


   Waambie mabingwa wa matusi mitandaoni kuwa dawa yao inakuja na hivi karibuni mtambo huo utafungwa kwani tumeuagiza toka Africa kusini tu! Hatupo tayari kuona wizara yetu inakuwa ndio mfano kwa watu kutukana wasanii wetu ovyo ovyo, Inachukuliwa kama hatuna meno ya kuwamaliza hao wanaotukana...sasa wizara kupitia BASATA imeamua na itatoa mfano kwa hao wote wanaotengeneza Account feki kutukana watu au wasanii kila wakati.


      Nadhani wasomaji wangu mmeona na mmeelewa wazi wazi nini lilikuwa lengo la kuniita pale Basata na sababu kubwa aliyosema ni kuwa hataki jina lake liandikwe mtandaoni amesema kuwa yeye sio msemaji wa wizara hivyo sivyema kwani kila sehemu kuna taratibu zake katika kufikisha lile tamko la wizara au sehemu husika kwa wakati husika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni