NA KAIS MUSSA KAIS.
Asalaam aleykum ndugu wasomaji wangu wapendwa, leo siku ya alhamisi nawaletea kile kipengele cha "Ninavyojisikia" kumbuka kuwa segment hii itakuwa ikiwajia kila alhamisi panapo uhai na uzima.
VIJANA WA JAGWA WAKIIMBA KWA HISIA KATIKA MOJA YA MATAMASHA YAO. |
Hapa nitakuwa nazungumzia muziki tofauti na taarab kama ambavyo tumezoea na hii nimeiweka makusudi ili tuweze kujifunza toka kwa wenzetu pia wamewezaje kupiga hatua mpaka kufikia walipo?. Kuna muziki wa pwani ambao umezoeleka zaidi kuchezwa uswahilini unaitwa mchiriku, lakini hapo zamani zaidi ulikuwa unatambulika kama mnanda! ila baada ya kuboreshwa zaidi na kuanza kupigwa kwa instrumental za kisasa ukabadilishwa jina na kuitwa mchiriku ijapokuwa bado mpaka leo wapo wanaoita muziki huo mnanda!.
Huu muziki kwa sasa nadiriki kusema wazi kwamba ni kitambulisho tosha cha nchi yetu ya Tanzania kwani nchi za ulaya zimekuwa zikivutiwa zaidi na muziki huu toka Tanzania kuliko muziki wowote ule!, vikundi vya mchiriku vimekuwa vikipata mialiko kadhaa wa kadhaa huko ughaibuni katika matamasha ya kimataifa zaidi na wanafanya vizuri karibia kila mwaka.
JAGWA MUSIC WAKIFANYA YAO NCHINI DERNMAK. |
Kikundi kama cha Jagwa music watoto wa mwananyamala kwa manjunju tayari wamekuwa nembo halisi ya Tanzania nje ya nchi kwani wameweza kushiriki matamasha mbalimbali katika nchi za Ujerumani, Dernmak, Sweden na Uholanzi, pia wamekuwa wakiuza CD zao kila wanapokuwa nje ya nchi na zimekuwa zikinunuliwa kwa kasi ya ajabu sana, huo ndio mchiriku muziki ambao serikali wameufumbia macho kwa kuuona ni muziki wa kihuni.
KIKUNDI CHA JAGWA MUSIC WAKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA. |
Lakini hapa ndugu wasomaji wangu cha kujiuliza ni kwamba,Pamoja na wanamuziki wa Tanzania kutoka uswahilini kuitangaza vyema Tanzania kuliko hata hao wanaolinga na kunata, lakini je serikali ya nchi yetu kwanini hawawathamini na kuwatengenezea mazingira mazuri ya utendaji kazi zao? Baadhi ya ngoma za asili kama mdundiko, vanga, ngoma ya unyago "msondo" zinazuiliwa eti za kihuni kwa ulimbukeni wa watu wachache kuiga vya kigeni na kusahau utamaduni halisi wa kitanzania! huu ni ujinga wa dhahili kabisa.
HII NDIO MASKANI YA JAGWA MUSIC MAENEO YA MWANANYAMALA. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni