Baraza la Sanaa
la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha
Msanii wa muziki wa dansi Ramadhan Ally Masanja (Banza Stone)
kilichotokea nyumbani kwao Sinza jijini Dar es Salaam jana mchana siku ya
Ijumaa ya tarehe 17/07/2015 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Banza Stone ni msanii na mdau wa
muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa na mchango mkubwa katika
kukuza muziki wa dansi nchini hasa katika kubuni miondoko mbalimbali
ambayo ilikuja kupata umaarufu mkubwa. Moja ya mwondoko uliopata
umaarufu mkubwa ni ule wa “Achimenengule” akiwa na Bendi ya Tanzania One
Theatre (TOT).
BANZA STONE ENZI ZA UHAI WAKE. |
Mchango wake katika muziki wa
dansi hasa katika kubuni na kutunga nyimbo zenye ubora, ujumbe na
maadili kwa jamii hautasahaulika kamwe. Ni mwanamuziki aliyeacha misingi
katika sekta ya muziki na alijitolea kwa kiasi kikubwa katika
kuufikisha muziki wa dansi mahali ulipo leo.
Itakumbukwa kwamba mnamo Julai 3,
2015 BASATA na Asha Baraka, Mkurugenzi wa African Stars Entertainment
(ASET) walichukua juhudi za makusudi kwenda nyumbani kwa msanii huyu
kufanya mashauriano na familia yake ikiongozwa na kaka yake Khamis Ally
Masanja na hatimaye kwa pamoja kumrejesha tena hospitalini kwa ajili ya
matibabu yake.
Hata hivyo pamoja na juhudi hizo
za kupigania uhai wake Mungu kampenda zaidi Msanii mwenzetu Banza Stone.
Upendo wetu kwake umezidiwa na ule wa mwenyezi Mungu ambaye kimsingi
wote tutarejea kwake.
BANZA STONE WAKATI AKIUMWA!. |
Baraza, wasanii na wadau wote wa
Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu Banza
Stone hasa katika kupenda kujitolea muda mwingi katika kukuza muziki wa
dansi na sekta ya muziki kwa ujumla.
Baraza linatoa pole kwa ndugu wa
marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na wadau wote wa Sanaa katika
kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni