TANGAZA NASI

Breaking

Jumanne, 20 Oktoba 2015

JE UNAWAJUA TAUSI WOMEN TAARAB KUTOKA VISIWANI ZANZIBAR?...SOMA HABARI KAMILI HAPA!.

NA KAIS MUSSA KAIS.


                            TAUSI ni mmoja wa ndege maarufu ambae ni mrembo alieumbika kutokana na umbo lake zuri la kupendeza,uzuri huo pia huonekana kwa manyoya yake ambayo pia ni kivutio kwa wengi wakiwemo watoto wadogo.


Nyimbo mbali mbali ziliwahi kuimbwa ambazo zinaonyesha kumsifia ndege huyo na kuonekana kuvuta mapenzi kwa watu wengi,lakini pia uzuzri wa ndege huyo kumefanya hata kupatikana kwa jina la la mtu kwa uzuri wake.


Lengo langu sio kumsifia wala kumzungumzia ndege huyo ,bali ni kuzuzngumzia mustakabali mzima wa kundi la taarab la akina mama ambalo limeweza kujizolea umaarufu mkubwa sana ndani nan je ya visiwa vya Zanzibar.


Mara baada ya kuona kazi zinazofanywa na akina mama hao mwanzo mwa mwezi huu katika tamasha la Sauti za Busara hamu na shauku kubwa ilinipata ya kutaka kujua kiundani azma na lengo la kuanzishwa kwa kundi hilo.


Niliweza kufika katika Makao Makuu ya Klabu hiyo yalipo katika maeneo ya Kisiwandui mkabala na Msikiti Mabati mjini Unguja na kukutana na Mkurugenzi wa kundi hilo Bi Maryam Hamdani.


Bi Maryam alinielezea tangu kuanzishwa kwake,walipofikia na matumaini ya baadae ya kundi hilo .


Tausi ni kikundi pekee nchini Tanzania kinachopiga muziki wa taarab asilia ambacho kinafanya shughuli zake zote kupitia akina mama wanaoongozwa na Mkurugenzi huyo anaepiga ala ya Qanoon.


Sio jambo la rahisi kuona akina mama hao wanaweza kufanya kazi hasa ya kupiga ala asilia ambazo ni ngumu kutokana na ala hizo kutumika bila ya umeme na ndio jambo lililonifanya niamini kwamba wanawake wakiamua wanaweza.


Jina la Tausi limetokana na Mkurugenzi huyo kumpenda ndege huyo tangu akiwa mdogo na alisema kuwa mapenzi yake yalikuwa kwa ndege wawili ambae ni Tausi na Ziwarde na ndipo akaamua kukiitia kikundi hicho kwa jina la Tausi.


“Tangu utoto wangu Tausi na Ziwarde nilikuwa nawapenda sana nikaamua nikaamua kukiita kikundi hichi jina la ndege huyu na pia nilitaka kubadilisha majina ya vikundi vya taarab na sio kila siku hayo kwa hayo,”alisema Bi Maryam.


Tausi ilizaliwa rasmin Julai mwaka 2009 kikiwa na vijana wa kike 22 ambapo alianza nao kwa kuwafundisha kupiga ala mbali mbali akiwa yeye na walimu wenzake Marehemu Iddi Abdallah Farahan,Mohammed Ilyas,Ramadhan Muhidin na Ali Ibrahim.


Walianza kwa kuwafundisha kutumia ala mbali mbali ikiwemo Qanoon,Udi,Fidla,Violin,Tablah,Key board, Bongos na aina mbali mbali za ala ambazo zinatumika katika muziki wa taarab asilia.


“Hamu yangu ya kupenda muziki wa taarab na mimi mwenyewe nikiwa msanii na pia nafahamu kutumia ala ya Qanoon ndio niaamua kuanzisha kikundi hichi ambapo nilianza na akina mama 22,”alisema.


Mara baada ya kuonekana kwamba upo umuhimu kutokana na kuanzishwa kwa kikundi hicho watu mbali mbali wenye hamu ya kuwa wasanii ambao wanahitaji kujifundisha kutumia ala walianza kujiunga na Tausi.


Mkurugenzi huyo anafahamisha kwamba sharia ya kikundi hicho kuwa hakuna msanii yoyote aliekuwemo ndani ya Tausi lazima ajue kupiga ala na sio kubakia kwenye kuimba tu.


“Wapo wasanii ambao walijiunga na Tausi wakiwa hawajuai chochote zaidi ya kuimba tu,lakini nashukuru kutokana na jitihada ya Tausi na sharia yetu watu wote wajue kupiga ala basi sasa hivi takriban wasanii wetu wote wanajua kutumia ala,”alifahamisha.


Hakuna jambo lizilokuwa na matatizo wala faida,lakini kwa upande wa matatizo yanayokikabili kikundi hicho ni ukosefu wa vifaa ikiwemo kukatika kwa  nyuzi ambazo zinatumika kwenye ala na matatizo mengine amabayo alisemani ya kawaida tu.


Lakini kwa upande wa faida,Tausi imeweza kupata faida mbali mbali ikiwemo kujua kupiga ala,kujiajiri wenyewe kujua zaidi kutumia ala za asili,kupiga taarab katika sehemu mbali mbali na kuweza kusafiri.


Mkurugenzi huyo alizitaja sehemu ambazo wamebahatika kufanya maonyesho ni katika matamasha ya busara kwa miaka mitatu,sherehe za mkutano wa EU sherehe za chakula cha usiku kwa wadau wa elimu pamoja na uzinduzi wa mkutano mkuu wa AU uliofanyika mjini Nairobi na kuhudhuriwa na alikekuwa Makamo wa Rais wan chi hiyo Raila Odinga.


Lakini pia Mkurugenzi huyo alisema kujwa faida nyengine kwa kundi hilo ni kuhudhuria katika matamasha ya kimataifa yaliofanyika nchini Lebanoon na Misri.


“Hii ni faida kwetu na faraja iliyoje kupata kufanya maonyesho katika sehemu mbali mbali tena kubwa ambazi imeweza kutusaidia kukitangaza kikundi chetu pamoja na nchi yetu kwa ujumla,”alieleza.


Aidha kundi hilo pia limeweza kupiga nyimbo mbali mbali pamoja na Bashraf zao wenyewe ambazo zimetungwa katika kundi hilo ambapo miongoni mwa watunzi hao akiwa yeye mwenyewe Mariam Hamdani.


Tausi linatamba na nyimbo zake mbali mbali zikiwemo Usione vyaelea,Walodhani mzaha,Nibembeleze,Si rahisi na dhana ambapo kwa upande wa bashraf zinajuliakana kwa jina la Tausi na Alya.


“Kundi letu limeweza kutunga nyimbo pamoja na bashraf  ambapo tunapokwenda katika maonyesho huwa tunapiga nyimbo zetu wenyewe,”aliongezea Mkurugenzi huyo.


Aidha kwa upande wa matarajio ya kikundi hicho Maryam alisema ni matarajio yao kuwasomesha wasanii wa kundi hilo ndani nan je ya Zanzibar ili waweze kuwa wasanii watakaoitangaza vyema Zanzibar.


“Matarajio yetu Tausi ni kuwapa mafunzo yalio bora wasanii wetu ambayo watayapata ndani nan je ya Zanzibar ili wawe wasanii bora ambao wataitangaza Zanzibar kupitia fani hii ya muziki wa Taarab asilia,”alisema.


Mbali na hayo lakini pia malengo mengine ya Tausi ni kupata wasanii bora wa kike ambao ambao wataweza kutunga mashairi ambayo yatasaidia kuwainua wanawake na pia kutafuta klabu maalum .


Alifahamisha kwamba lengo la kutafuta klabu ni kutaka kuendelea kwa kikundi hicho ambapo alifahamisha kwamba vikundi vingi  sana vya taarab vinakufa kutokana na kukosekana kwa klabu .


Maryam Hamdani ambae pia ni Makamo wa Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT)  amewashauri wasanii kuendeleza muziki wa taarab asilia ili waweze kuitangaza nchi yao kupitia fani hiyo.


Pia aliwashauri wanawake kutumia fani hiyo kuwa ni ajira na sio kuifanya fani hiyo kuonekana kuwa ni fani ya kihuni jambo ambalo alisema kuwa sio kweli bali ni dhana potofu kwa watu wasiopenda fani hiyo.


Kutokana na sababu mafanikio hayo,Mkurugenzi wa Tausi ambae pia ni mwanzilishi wa kundi hilo ana kila sifa ya kupewa kutokana na ujasiri wake alionao katika kusaidia kutetea haki za wanawake wenzake katika Nyanja ya muziki wa taarab.


Hii ni faraja kubwa kwa nchi yetu kutokana na mama huyo kuona umuhimu kundi hilo na hakuna budi kwa taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi kukisaidia kikundi hicho ili kiweze kukuwa na kuwapatia ajira akina mama hao.


Tausi ambalo ni kundi maarufu likiwa chini ya mlezi wake aliekuwa Waziri wa Fedha za zamani wa Jamuhuri ya Muungano wam Tanzania Zakia Meghji linaendelea kufanya maonyesho yake katika sehemu mbali mbali za mjini na mashamba... Makala hii ni kwa hisani ya Bin Mahmoud.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni