NA KAIS MUSSA KAIS.
KWENYE miaka ya hivi karibuni kumekuwa na jitihada
zenye mwelekeo potofu katika vyombo vya habari mbalimbali kupotosha
maana na dhana halisi ya taarabu na kile ambacho taarabu inastahili kuwa
na kuitwa.
Baada ya Watanzania kugeuka wavivu wa kila kitu ikiwemo kupiga ala za
muziki na kutaka mteremko katika kila jambo wale waliozuka na mitindo
inayotumia mashairi, au tungo zenye vina na mizani, au isivyo hivyo
wakaona urahisi ni kuita miziki yao 'modern taarab'. Miziki hiyo
ninakaata sio taarabu bali inastahili kuitwa mipasho, kiduku, rusha na
roho, au mnanda na vitu kama hivyo, lakini kamwe sio taarabu.
Muziki wa taarabu una asili na fasili yake katika watu wa Pwani na
visiwani na maeneo ya mwambao wa Afrika Mashariki.Umeathirika kwa kiasi
kikubwa na muziki wa Mashariki ya Kati, India na kaswida za Kiislamu.
Sifa moja kubwa ya muziki wa taarabu tofauti na wengi wanavyofikiri sio
maneno na mpangilio wake, bali ala za muziki huo na mipangilio yake na
ule ufundi wa kila mwanataarabu kuwa bingwa au stadi katika kupiga
chombo fulani. Taarabu isipokuwa na ala hizi sio taarabu ni igizo tu
kwa kiasi fulani la kitu kama taarabu. Taarabu kwa kawaida ni kitulizo
cha fikra ndani ya nyumba na katika hadhara isiyoshawishiwa na usasa na
umagharibi kiasi cha kupuuza maadili na mila za wahusika.
Ala za taarabu ni nyingi na swahiba wangu Mbaraka albela ambaye sio tu
shabiki wa taarabu bali ni mtunzi pia wa nyimbo za taarab anaweza
baadaye kunipokea hapa na kuelezea zaidi kwanini tunastahili kuwekeza
kwenye taarab asilia, kama eneo la utamaduni linalostahili kuhifadhiwa
na kuenziwa.
Taarabu kama walivyoiendeleza kina Siti binti Sadi, Bi Kidude, Juma
Bhalo na kina Sheikh Ilyas, Machapurala bila kuwasahau mamia ya wanawake
na wanaume wa Kizanzibar na Kimrima waliochangia maendeleo ya tasnia
hii adimu, lakini iliyo na sifa ya kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa
mwambao ya Pwani ya Afrika Mashariki na usiostahili kuachiwa kupotea.
Taarabu ni muziki wa enzi na enzi. Ni sehemu ya utamaduni endelevu na
hususan katika mikoa ya pwani ya Afrika Mashariki. Taarabu ni
ustaarabu, utaratibu, upole na uungwana. Taarabu ni kitulizo cha mawazo
na gundi ya kuunganisha familia kama sio ukoo mzima. Sifa ambayo si
mipasho, sio rusha roho sio mnanda unayo.
Taarabu kiasili sio muziki wa kucheza bali wa kutazama, kusikiliza,
kutafakari na kutunza. Huu ni muziki uliokuwa ukisikilizwa na watu wenye
fikira, busara na hekima kuwapa muda wa kuwaza na kuwazua juu ya hili
au lile. Muziki wa kupayuka, kujiona, mshauzi, kusemana, kutukanana,
kuumbuana na wenye nyimbo ambazo hazina staha, usiri wala taadibu ya
kuimbwa katika mafumbo hauwezi kuitwa taarab.
Ni muziki ambao kwa kawaida una ala takriban ya ishirini. Na kwa wapenzi
halisi wa taarabu hufuatilia upigaji wa kila ala na ufundi au ugwiji wa
yule anayetumia ala husika. Aidha, mashairi ya taarab hayaangalii tu
mlingano wa vina na mizani bali maudhui na mantiki ya kile kilichomo
tena kikiwa kwenye mafumbo kuweza kusomeka vyema na wanaosikiliza wimbo
husika.
Ni muziki ambao hutungwa kwa mafumbo na kwa namna ambayo hauzui familia
nzima, yaani, babu, bibi, baba, mama, kaka na dada wote kujumuika kwa
pamoja bila kutokea chochote ambacho kinaweza kuwafanya washindwe
kuzungumza au kutazamana. Taarab kiasili uliunga pamoja familia za
wakazi wa mji husika. Tofauti na hiyo inayoitwa 'modern taarab' ambayo
kwa kiasi kikubwa inazivunja familia katika kila mji na kijiji.
Siti bint Saad (1928) ndiye nyota wa kwanza wa taarab ambaye kwa mara
ya kwanza badala ya kuimba kwa Kiarabu aliimba kwa Kiswahili. Alifyatua
mamia ya santuri za nyimbo India na wapenda muziki wa enzi hizo hakuna
aliyekosa wimbo wake nyumbani.
Muziki wa taarab asili hauna tofauti na 'Classical Music' wa Ulaya au
'Country Music' wa Marekani. Miziki hiyo ilikuwepo, imekuwepo na
itakuwepo bila kubadilika wala kuitwa kwa jina jingine wala kupigwa kwa
namna nyingine tofauti na ilivyokuwa, ilivyo sasa na itakavyokuwa kesho.
Ni sehemu ya kudumu ya utamduni wa watu na sio kitu cha kupita na
kusahaulika.
Aina hizo za miziki pamoja na kuzuka kwa miziki ya kila aina Ulaya na
Marekani bado inatambulika kwa nembo na jina lake. Country ni country na
classical ni classical. Hapajakuwapo muziki mwingine uliopewa umodern
kuhusiana na miziki hii, hakuna kitu kama modern country au modern
classic.
Rouget katika Music and Trance anafafanua kwamba neno taarabu
linatokana na neno la kiarabu 'tariba' likiwa na maana ya hisia za
kusisimka, kudhihirisha au kutaka kufanya kitu Fulani, kama vile kuimba
au kucheza taarab.
Kama jitihada zinavyofanyika kukarabati na kutunza maeneo kama vile Mji
Mkongwe Zanzibar, Bagamoyo na Kilwa ili iendelee kuwepo basi upo
umuhimu pia wa wanaohusika katika serikali zetu kuhakikisha kuwa muziki
wa taarab asili na wanamuziki wake wanakumbukwa na kuenziwa na kisha
kizazi kipya kinajengwa ili kuendeleza muziki huu kwa faida ya vizazi
vijavyo. Kwa maana, ukweli ni kwamba taarabu asili ikipotea ndio utakuwa
mwisho wa taarabu hapa Afrika Mashariki.
Kwanini tuhifadhi taarab asilia
Kwa bahati mbaya wengi tumezoea kuchukulia vitu kama ardhi, fedha,
nyumba, magari kuwa ndio rasilimali tu. Lakini muziki wa kiasili nao ni
rasilimali muhimu kimaendeleo na kisaikolojia. Bila urithi wa namna hii
tutakuwa ni taifa lipolipo tu ambalo si jambo zuri.
Pamoja na mambo mengine kuifufua, kuitunza na kuiendelza taarab asili ni
jambo lenye faida kadhaa ikiwemo kuendeleza mila na utamaduni wetu,
kuzileta familia pamoja mara kwa mara, kujenga maadili bora katika
jamii, kuwa na muziki usioendana kinyume na maadili ya dini, kukuza na
kuendeleza ushairi na Kiswahili, kuwa kivutio kwa wageni wa leo na kesho
na kuzienzi na kuendeleza ala asili za muziki na upigaji wake.
Miziki inayojiita modern taarabu iitwe kwa majina yao yanayostahili kama
ni kiduku basi kiduku, au rusha roho basi rusha roho fulani, kama ni
mipasho basi ni ‘Mipasho’ na kama ni mnanda uitwe ‘Mnanda’ na miziki hii
isiruhusiwe kutumia mgongo wa taarabu kujijenga isipostahili.
Ninawashauri wanaharakati wa kulinda na kuendeleza utamaduni wetu
kuangalia uwezekano wa haya yafuatayo: Kusaidia juhudi binafsi zilizopo
za kufufua na kuendeleza vikundi vya taarabu kupitia vilabu na vyuo vya
upigaji ala za asili za taarab (mathalani juhudi za Bi Hamndani,
Zanzibar), Kushirikiana na Unescokuhifadhi taarabu asili kwa kutumia
Teknohama; Kuwatafuta wanataarab asilia waliko na kuwaunganisha ili
kuufufua na kuchochea kuwepo kwa muziki huo kiasili na kuongeza vionjo
viwili vitatu vya kuvutia familia zaidi kuliko mtu mmoja mmoja.
Aidha, kusaidia vikundi vilivyopo, lakini havina ala za kutosha za
muziki toka Misri na Uarabuni, kuenzi Ushairi katika vyombo vya habari
kukuza vipaji vya washairi chipukizi na kuchukulia Taarabu asili kama
urithi usiostahili kupotea kwa msaada wa Unesco na wapenda utamaduni
wetu wengineo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni